Jul 13, 2016 18:29 UTC
  • Amnesty: Mamia wametoweka mikononi mwa vyombo vya usalama Misri

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeeleza wasiwasi wake juu ya wimbi la kutoweka mamia ya watu wakiwa mikononi mwa vyombo vya usalama nchini Misri tangu mapema mwaka jana.

Philip Luther, Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amesema kwa wastani watu watatu hadi wanne wanaoonekana kuwa wapinzani na wakosoaji wa serikali wanatoweka kila siku nchini Misri. Luther amesema serikali ya Cairo inatumia sera hiyo ya kuwateka nyara na kuwakandamiza wakosoaji wake kwa shabaha ya kuwanyamazisha kimya.

Ripoti ya Amnesty International imesema kuwa, aghalabu ya wanaokamatwa, kuzuiliwa katika mazingira ya kutisha na kukandamizwa ni wafuasi wa rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya demokrasia, Muhammed Morsi ambaye alipinduliwa Julai 2013.

Ripoti ya shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu imeongeza kuwa, vyombo vya usalama nchini Misri vinatumia kisingizio cha 'kupambana na ugaidi' kuwakamata na kuwakandamiza wapinzani, wanaharakati na wakosoaji wa serikali wakiwemo wanafunzi wenye chini ya umri wa miaka 14.

Watetezi wa haki za binadamu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika wanasema kwa akali watu 1,400 wameuawa, 22,000 wamekamatwa ambapo 200 miongoni mwao wamehukumiwa vifo katika operesheni za maafisa usalama nchini humo za kuzima maandamano na malalamiko ya wananchi tangu mapema mwaka jana 2015.

Tags