Jul 14, 2016 15:50 UTC
  • Umoja wa Mataifa wasikitishwa na uvunjaji wa haki za binadamu DRC

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa imeelezea kusikitishwa kwake na kuendelea vitendo vya uvunjanji wa haki za binadamu nchini Kongo na kusema kuwa, zaidi ya kesi elfu mbili za uvunjaji wa haki za binadamu zimeripotiwa nchini humo katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na ofisi hiyo inayojulikana kwa kifupi kwa jina la BCNUDH imesema kuwa, kesi 2,343 za uvunjaji wa haki za binadamu ambao ni wastani wa kesi 390 kwa kila mwezi, zimeripotiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, idadi hiyo imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kesi zilizoripotiwa katika muda kama huo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya haki za binadamu ya mjini Kinshasa, watu wanaofanya vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu ni wanajeshi na polisi wa nchi hiyo pamoja na magenge ya watu wenye silaha.

Sehemu kubwa ya uvunjaji huo wa haki za binadamu unafanyika katika maeneo yenye machafuko ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi wasiopungua 79 na polisi 35 wanakabiliwa na tuhuma za kufanya vitendo vilivyo dhidi ya binadamu huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tags