Jun 13, 2024 02:24 UTC
  • Chama cha Zuma kususia kikao cha Bunge cha kumchagua rais wa Afrika Kusini

Chama cha upinzani cha Mkhonto weSizwe (MK) cha rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kimewasilisha faili mahakamani kikitaka kusikitishwa kikao cha Bunge cha kuchagua rais mpya wa nchi hiyo.

Chama hicho ambacho ni moja ya vyama vikubwa vya upinzani Afrika Kusini kimesema Wabunge 58 waliochaguliwa katika uchaguzi wa hivi karibuni kupitia chama hicho hawatashiriki kikao hicho cha Ijumaa, cha kuchagua rais wa nchi.

Hapo awali, chama hicho kilichukua hatua nyingine ya kisheria ya kuizuia Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo (IEC) kutangaza matokeo ya uchaguzi huo mkuu, lakini bila mafanikio.

Kiliwasilisha 'ithibati na vielelezo' mbele ya IEC, kuonyesha kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro nyingi. Aidha vyama vingine vya upinzani vikiongozwa na Democratic Alliance (DA) vilisema ujumlishaji wa matokeo katika baadhi ya maeneo hasa katika mkoa wa Western Cape ulikumbwa na mizingwe na uchakachuaji, na hivyo kutaka kura zihesabiwa upya.

Bunge la Afrika Kusini

Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na IEC, chama tawala ANC kiliongoza katika uchaguzi wa Bunge wa mwishoni mwa Mei, kwa kuzoa asilimia 40 ya kura, kikifuatiwa na chama cha Democratic Alliance (DA) kilichozoa asilimia 21.75, huku chama kipya cha Mkhonto weSizwe (MK) cha Zuma kikiambulia asilimia 14 ya kura.

Chama cha ANC, ambacho kilikuwa kikipata zaidi ya 60% katika chaguzi zote tangu 1994, isipokuwa 2019, wakati ushindi wake ulipopungua hadi 57.5%, kilipata 40.18% tu ya kura katika uchaguzi wa mwaka huu. Hali hiyo imekiweka chama hicho katika wakati mgumu kuweza kuunda serikali peke yake, na hivi sasa kipo mbioni kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Tags