Jun 17, 2024 10:49 UTC
  • AU yakabidhi kambi nyingine kwa Somalia katika awamu ya 3 ya kuondoka kijeshi

Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika (AU) nchini Somalia (ATMIS) kimetangaza kwamba kimekabidhi kambi ya kijeshi ya Barire kwa vikosi vya usalama vya Somalia ikiwa ni kuashiria kuanza awamu ya tatu ya kuondoa wanajeshi wake nchini humo.

Kikosi hicho kimesema kuwa, kambi hiyo ambayo iko katika eneo la Lower Shabelle chini ya usimamizi wa Jeshi la Ulinzi la Uganda tangu mwaka 2019, ina umuhimu mkubwa wa kimkakati kwani inafanya kazi ya kusimamia usalama wa eneo lenye ukubwa wa takriban kilomita 60 magharibi mwa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Kamanda wa Kikosi cha ATMIS cha Uganda, Anthony Lukwago Mbuusi amesema katika taarifa iliyotolewa mjini Mogadishu kwamba, hatua hiyo inaashiria kupatikana maendeleo katika jitihada za pamoja za kurejesha amani ya kudumu nchini Somalia.

Wakati akikabidhi kambi hiyo ya kijeshi kwa Muhudin Ahmed, mwakilishi wa Jeshi la Taifa la Somalia (SNA), Mbuusi amesema: "Tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja kuelekea kwenye mustakabali mzuri wa Somalia, utakaokuwa umejengwa juu ya ushirikiano kuheshimiana na kwa ajili ya kufanikisha lengo la pamoja la kutafuta amani ya kudumu."

Kwa upande wake, Muhudin Ahmed amewashukuru wanajeshi wa ATMIS wa Uganda kwa kujitolea kwao katika kipindi cha mpito na kujitolea kwao katika kuhakikisha amani inarejea Somalia.

Ujumbe wa AU uliondoa wanajeshi 5,000 nchini Somalia na kukabidhi kambi 17 za kijeshi kwa Vikosi vya Usalama vya Somalia wakati wa awamu ya kwanza na ya pili ya kuondoka kijeshi nchini humo, zoezi ambalo lilikamilika mwaka jana 2023.

Awamu ya tatu ya kupunguzwa wanajeshi wa ATMIS inafanyika kwa mujibu wa maazimio nambari 2628 (2022), 2670 (2022), na 2710 (2023) ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambayo yanaiamuru ATMIS kuondoa wanajeshi 4,000 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Juni.

Tags