Ecowas yamteuwa Rais wa Senegal kuzungumza na Burkina Faso, Mali na Niger
(last modified Tue, 09 Jul 2024 02:24:19 GMT )
Jul 09, 2024 02:24 UTC
  • Ecowas yamteuwa Rais wa Senegal kuzungumza na Burkina Faso, Mali na Niger

Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) imemtaka Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye kushirikiana na nchi tatu wanachama wake wa zamani zinazoongozwa kijeshi kujaribu kuliunganisha eneo hilo ambalo utulivu wake umekuwa hatarini tangu zilipoamua kujitoa katika jumuiya hiyo mwezi Januari mwaka huu.

Katika mkutano wake huko Abuja mji mkuu wa Nigeria, Ecowas imemteua Rais Bassirou Faye wa Senegal kuwa Mjumbe wake katika mazungumzo na watawala wa kijeshi wa Mali, Niger naBurkina Faso. Itakumbukwa kuwa nchi hizo tatu zimeasisi Muungano wao wa Sahel baada ya mapinduzi yaliyojiri katika nchi hizo kuibua mvutano katika uhusiano na majirani zao. 

Omar Alieu Touray Mkuu wa Kamisheni ya Ecowas amesema kuwa ajenda za mazungumzo hayo bado hazijawekwa wazi. 

Omar Alieu Touray 

Mali, Niger na Burkina Faso zilisema juzi katika mkutano wao kuwa wameipa kisogo kikamilifu jumuiya ya Ecowas. Hii ni mara ya kwanza katika historia yake ya karibu miaka 50 kushuhudia Ecowas ikipoteza wanachamawake namna  hii. 

Karim Manuel Mchambuzi wa masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati amesema kuwa jukumu  alilopewa Rais wa Senegal ni kubwa kwa kuzingatia mivutano inayoendelea magharibi mwa Afrika hata hivyo ni jambo lililo mbali jitihada zake kuzaa matunda hivi karibuni.

Wakuu wa Jumuia ya  ECOWAS walisemajana katika taarifa yao huko Abuja Nigeria kuwa shirikisho lililoundwa  kati ya Mali, Niger na Burkina Faso ni changamoto kuu kwa jumuiya hiyo ambayo inakabiliwa na matatizo mbalimbali kama ukosefu wa bajeti, uhalifu wa makundi ya wanamgambo wenye silaha n.k.