Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amtaka Machar arejee mjini Juba
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amemtaka Riaek Machar, Makamu wake wa Rais kurejea mjini Juba, mji mkuu wa nchi hiyo na kwamba njia hiyo itasaidia kurejesha usalama mjini hapo.
Rais Kiir aliyasema hayo jana Alkhamis na kuongeza kama ninavyonukuu: "Ninamtaka Machar arejee mjini Juba ili tuweze kuendeleza utekelezaji wa makubaliano ya amani, kwani utekelezaji wake unahitaji uepo wake." Mwisho wa kunukuu. Kadhalika Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ameahidi kudhamini usalama wa Machar wakati wa kurejea kwake mjini Juba.
Kwa mujibu wa Rais Kiir, anasubiria kwa kipindi cha masaa 48 hadi kufanya mawasiliano ya kuanza kuchukua hatua za kuimarisha usalama na amani baina ya raia wa nchi hiyo ambao hadi sasa wanapitia kipindi kigumu. Hii ni katika hali ambayo Riek Machar alitoweka mjini Juba, tangu kuliposhadidi mapigano mjini hapo. Machafuko mjini Juba yaliibuka tarehe saba mwezi huu ambapo hadi sasa kwa akali watu 300 wameripotiwa kuuawa. Aidha machafuko hayo yameathiri makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwaka jana 2015 kati ya mahasimu hao wawili.