Oct 06, 2024 02:28 UTC
  • Chad yatoa indhari ya janga baya zaidi la mafuriko

Serikali ya Chad imetangaza indhari ya janga bayya zaidi la kimaumbile la mafuriko baada ya mito kadhaa kufurika nchhini humo.

Kulingana na Waziri Mkuu wa Chad, Allamaye Halina, mto Chari umefurika mita nane zaidi ya kiwango chake katika kipindi cha siku kumi zilizopita.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, mafuriko makubwa yaliyoikumba Chad ambayo yamekuwa yakishuhudiwa tangu Julai, tayari yamewaathiri zaidi ya watu milioni 1.7, kuharibu nyumba laki moja na sitini na nne elfu na ekari laki mbili na hamsini elfu za mashamba.

Zaidi ya watu 500 wanaripotiwa kupoteza maisha nchini Chad kufuatia mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.

Mafuriko Chad

 

Marcelin Kanabé Passalé, Waziri wa Maji na Nishati wa Chad amesema, mvua hizi zimesababisha mafuriko makubwa ambayo yameathiri majimbo yote ya nchi, na kusababisha mamia ya watu kupoteza maisha lakini pia uharibifu mkubwa wa mkiuundombinu na mifugo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) nchini Chad imetangaza kuwa, mvua zinazoendelea kunyesha nchini Chad tangu mwezi Julai zimesababisha vifo vya watu 503 na kuathiri zaidi ya watu milioni 1.7.

Umoja wa Mataifa ulionya mwanzoni mwa mwezi huu wa Septemba kuhusu athari za "mvua kubwa na mafuriko makubwa" katika kanda hiyo, hasa nchini Chad, na kutoa wito wa kuchukuliwa "hatua za haraka na ufadhili wa kutosha" iili  kukabiliana na "mgogoro wa hali ya hewa".