UNHCR: Raia wengi wa Sudan Kusini wamekimbilia nchini Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11746-unhcr_raia_wengi_wa_sudan_kusini_wamekimbilia_nchini_uganda
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, machafuko ya hivi karibuni nchini Sudan Kusini, yamewafanya raia wengi wa nchi hiyo kukimbilia nchini Uganda.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2016 03:33 UTC
  • UNHCR: Raia wengi wa Sudan Kusini wamekimbilia nchini Uganda

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, machafuko ya hivi karibuni nchini Sudan Kusini, yamewafanya raia wengi wa nchi hiyo kukimbilia nchini Uganda.

Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, zaidi ya raia elfu 10 wa Sudan Kusini walikimbilia nchini Uganda katika kipindi cha mapigano ya hivi karibuni. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia kubwa ya wakimbizi hao walioingia Uganda, walikuwa wanakabiliwa na njaa kali.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

 

Aidha shirika hilo limeongeza kuwa, tangu kulipoibuka machafuko nchini Sudan Kusini, jumla ya raia wa taifa hilo changa zaidi barani Afrika waliokimbilia nchi jirani ya Uganda wamefikia elfu 18 na 149. Mji mkuu wa Juba ulikumbwa na machafuko, mnamo tarehe saba ya mwezi huu, baada ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomuunga mkono makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar kupambana vikali ambapo kwa akali watu 300 wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Tayari Rais Kiir amemtaka Machar, kurejea mjini Juba, mji mkuu wa nchi hiyo kwa minajili ya kutekeleza makubaliano ya amani baina yao.