Iran na Tanzania zatia saini maelewano ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na viwanda
(last modified 2024-10-21T07:59:26+00:00 )
Oct 21, 2024 07:59 UTC
  • Iran na Tanzania zatia saini maelewano ya kuimarisha uhusiano wa kibiashara na viwanda

Hati ya Maelewano (MoU) katika nyanja za viwanda na biashara kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Muungano wa Tanzania imetiwa saini mwishoni mwa kikao cha tano cha Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Iran na Tanzania.

Makubaliano hayo yametiwa wino kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda na Ukarabati la Iran (IDRO) Farshad Moghimi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania Bi. Latifa M. Khamis.

Katika kikao hicho, pande hizo mbili zimetangaza utayari wao wa kufanya kikao katika siku za usoni ili kuunda mfumo wa kusaidia kufikia ushirikiano wa pamoja na kutekeleza makubaliano mbalimbali  ya ushirikiano wa pande mbili hizo.

Mahitaji mengi ya Tanzania ya viwanda yanahusiana na miundombinu ya usafirishaji, nishati, malighafi na mashine za viwandani, vifaa vya madini na dawa, amesisitza hayo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara ya Tanzania Bi. Latifa Khamis.

Kikao cha 5 cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran na Tanzania kilifanyika jaribuni hivi Dar es Salaam, mji mkuu wa Tanzania baada ya kusimama kwa miaka 16.

Katika kikao hicho, hati 11 za ushirikiano zimetiwa saini kati ya sekta binafsi za nchi hizi mbili ambazo zinaonyesha umakini maalum wa maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili kwa ajili ya kupanua ushirikiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali.

Kwa mujibu wa taarifa ya kikao hicho kikao cha 6 cha Ushirikiano wa Kiuchumi wa Pamoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran  na Tanzania kitafanyika mjini Tehran mwaka 2026.