Watu wasiopungua 39 wauawa katika mashambulizi ya waasi nchini Niger
Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa watu wasiopungua 39 wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wenye silaha magharibi mwa nchi hiyo karibu na mpaka na Burkina Faso.
Taarifa ya Wizara ya Ulinzi ya Niger imeeleza kuwa wahalifu wenye silaha wametekeleza hujuma mbili za kutisha katika jamii za Libiri na Kokorou ambao ni raia wasio na ulinzi. Hujuma hizo za kutisha zilifanyyika tarehe 12 hadi 14 mwezi huu wa Disemba huko magharibi mwa Niger.
Jamii za Libiri na Kokorou zinapatikana katika mkoa wa mpakani wa Tera; eneo ambalo limejaa wanamgambo wenye silaha ambao katika siku za hivi karibuni, wamekuwa wakitekeleza mashambulizi ya umwagaji katika maeneo mbalimbali.
Ardhi ya mpakani kati ya Niger, Mali na Burkina Faso kwa muda mrefu imekuwa maficho ya magaidi wenye mfungamano na kundi la Daesh na mtandao wa Al Qaeda, ambao wamekuwa wakiendesha vita vya uasi dhidi ya serikali.
Mapema mwezi huu wa Disemba, wanamgambo wenye silaha huko Niger walishambulia msafara wa magari uliokuwa umepakia bidhaa mbalimbali na kuuwa raia 21.