Nigeria yakanusha madai ya kula njama ya kuyumbisha amani huko Niger
Nigeria imekanusha "kwa matamshi makali sana" tuhuma za Niger kwamba inapanga njama ya kuyumbisha nchi hiyo kwa kuwasaidia wanamgambo waliofanya mashambulizi kwenye bomba muhimu la mafuta la nchi hiyo.
Hii ni baada ya Niger kumwita kumsaili Balozi mdogo wa Nigeria nchini humo ikiituhumu nchi hiyo jirani yake kwa kutumika kama kituo kikuu cha kuibua machafuko huko Niger.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria imesema katika taarifa yake kuwa serikali ya Nigeria inatoa pole kwa serikali ya Niger kwa shambulio la bahati mbaya katika bomba la mafuta lakini inaeleza kuwa wahalifu hawakuungwa mkono wala kusaidiwa na mamlaka za Nigeria.
"Serikali ya Nigeria imedhamiria kwa dhati kupambana na ugaidi na haitakubali au kuunga mkono vitendo vya makundi kama hayo "imeongeza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria.