Kesi 290 za kipindupindu zaripotiwa Sudan Kusini
Wizara ya Afya Sudan Kusini imethibitisha kutokea mripuko wa kipindupindu nchini humo huku kesi karibu 300 za ugonjwa huo zikiripotiwa.
John Rumunu, Mkuu wa Idara ya Kuzuia Magonjwa katika Wizara ya Afya ya Sudan Kusini amesema kesi 291 za ugonjwa huo zimeripotiwa kufikia sasa na kwamba 253 zimeripotiwa katika miji ya Juba na Terekeka. Ameongeza kuwa, visa 46 vya maambukizi ya maradhi hayo vimeripotiwa katika kaunti ya Duk jimbo la Jonglei.
Mkuu wa Idara ya Kuzuia Magonjwa katika Wizara ya Afya ya Sudan Kusini amewataka raia wa nchi hiyo kuchukua hatua za dharura kwa ajili ya kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa huo ambao umeenea kutokana na watu kutumia maji machafu ya Mto Nile mbali na kula vyakula kwenye mabanda ya wazi.
Julai 19, Makur Matur Koriom, Naibu Waziri wa Afya nchini humo alitangaza kuwa, zaidi ya watu 100 wamekumbwa na ugonjwa huo na kwamba hadi sasa watu 11 wamepoteza maisha kutokana na maradhi hayo. Kwa mujibu wa Matur Koriom, ongezeko la ugonjwa huo limetokana na mapigano ya ndani yanayoendelea nchini humo.