Sudan Kusini yakanusha tetesi za kuuawa Machar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12127-sudan_kusini_yakanusha_tetesi_za_kuuawa_machar
Sudan Kusini imekanusha tetesi kwamba kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo Riek Machar ameuawa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 28, 2016 00:21 UTC
  • Sudan Kusini yakanusha tetesi za kuuawa Machar

Sudan Kusini imekanusha tetesi kwamba kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo Riek Machar ameuawa.

Balozi wa Sudan Kusini nchini Kenya Jimmy Deng Makuach amekanusha madai hayo akisema kuwa ni propaganda zinazoenezwa na wafuasi wa Machar. Amesema serikali ya Juba haina nia ya kumuua Rielk Machar na kwamba kama ingetaka kumuua basi ingefanya hivyo katika machafuko yaliyoibuka hivi karibuni nchini humo. Balozi Makuach amesisitiza kuwa askari wa serikali ndio waliomsindikiza Machar hadi kwenye makazi yake wakati machafuko yalipoibuka nchini humo hivi karibuni.

Riek Machar ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini hajaonekana hadharani tangu kulipotokea machafuko mjini Juba ambayo yamepelekea kuua watu wasiopungua 300 hadi sasa na kutishia kuzusha tena vita vya ndani huko Sudan Kusini.

Mahasimu wawili Kiir na Machar

Baada ya machafuko hayo Rais Salva Kiir alimfuta kazi makamu wake, Riek Machar na kumteua Jenerali Taban Deng Gai kushika wadhifa huo.

Jenerali Gai alikuwa mkuu wa timu ya mazungumzo ya chama cha SPLM na Waziri wa Madini katika serikali ya mpito.