UNHCR: Maelfu ya wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya wamerejea kwao kwa hiari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12202-unhcr_maelfu_ya_wakimbizi_wa_kisomali_nchini_kenya_wamerejea_kwao_kwa_hiari
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, maelfu ya wakimbizi wa Somalia huko nchini Kenya wamerejea kwao kwa hiari.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 29, 2016 03:35 UTC
  • UNHCR: Maelfu ya wakimbizi wa Kisomali nchini Kenya wamerejea kwao kwa hiari

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa, maelfu ya wakimbizi wa Somalia huko nchini Kenya wamerejea kwao kwa hiari.

Taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya wakimbizi imetangaza kuwa, kuanzia Disemba mwaka 2014 hadi sasa jumla ya wakimbizi 18,287 wa Kisomali waliokuwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab iliyoko kaskazini mashariki mwa Kenya wamerejea kwa hiari nchini kwao.

Wananchi wa Somalia wakipokea misaada ya chakula

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, wakimbizi 12,177 kati yao walirejea nchini Somalia mwaka huu. Aidha imeelezwa kuwa, wakimbizi karibu elfu mbili ya idadi iliyotajwa wamerejea Somalia wakitokea Kenya kwa hiari yao tangu kuanza mwezi huu wa Julai.

Wakimbizi wa Kisomali wanaokuwa tayari kurejea kwao kwa hiari hurejeshwa kwa njia mbili za anga na barabara. Wakimbizi hao wanarejea nchini Somalia kwa hiari yao huku nchi yao ikiendelea kukabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kiuchumi na kiusalama.

Wanamgambo wa al-Shabab

Kundi la wanamgambo wa al-Shabab limeeendelea kuwa toshio la usalama wa nchi hiyo kutokana na mashambulio yake ya mara kwa mara.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, mapema mwezi huu, oparesheni ya kuwarejesha makwao wakimbizi wa kambi ya Dadaab ilianza licha ya kuwepo juhudi za kimataifa za kutaka kuzuia zoezi hilo. Imepangwa kuwa kambi hiyo ambayo inahesabiwa kuwa kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, itakuwa imefungwa kikamilifu kufikia mwezi Mei mwaka 2017.

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab, Kenya

Nusu ya wakimbizi wa kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni Wasomali waliokimbilia Kenya katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Kambi hiyo iko umbali wa kilomita mia moja kutoka kwenye mpaka wa nchi mbili za Kenya na Somalia.

Viongozi wa Kenya walitangaza kuwa wamelazimika kuifunga kambi hiyo kutokana na matatizo ya kiuchumi, kimazingira na kiusalama.