Jul 29, 2016 16:38 UTC
  • Jeffrey Feltman akihutubia Baraza la Usalama
    Jeffrey Feltman akihutubia Baraza la Usalama

Afisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameitolea wito kwa jamii ya kimataifa kuunga mkono pakubwa mapambano dhidi ya kundi la Boko Haram.

Jeffrey Feltman

Jeffrey Feltman amesisitiza katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kikosi kilichoundwa na Nigeria, Chad, Cameroon, Niger na Benin kwa ajili ya kupambana na kundi la Boko Haram kimefanikiwa kuwafurusha wanamgambo wa kundi hilo katika maeneo mengi. Hata hivyo amesema nchi za eneo la Ziwa Chad zinahitaji kuungwa mkono ipasavyo na jamii ya kimataifa ili kuweza kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo na vilevile kufanikisha vita dhidi ya Boko Haram. 

Nchi za eneo la Ziwa Chad 

Wakati huo huo Stephen O'bryan, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Anayehusika na Masuala ya Kibinadamu na Misaada ya Dharura amesema kuwa watu zaidi ya milioni tisa katika eneo la Ziwa Chad wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu. Amesema watu milioni mbili na laki nane kati ya hao waliotajwa wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kukimbia makazi yao wakihofia hujuma za Boko Haram.

O'bryan ameongeza kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinapasa haraka iwezekanavyo kuzidisha ushiriki wao katika mapambano dhidi ya Boko Haram katika eneo la Ziwa Chad na kujaribu kutatua mgogoro wa kibinadamu katika eneo hilo.

Tags