Ombi la mashirika ya utoaji misaada Sudan Kusini kwa Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12277-ombi_la_mashirika_ya_utoaji_misaada_sudan_kusini_kwa_umoja_wa_mataifa
Mashirika yanayofanya kazi ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuandaa mazingira ya ufikishaji misaada kwa waathirika wa vita vya ndani nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 30, 2016 10:26 UTC
  • Ombi la mashirika ya utoaji misaada Sudan Kusini kwa Umoja wa Mataifa

Mashirika yanayofanya kazi ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini Sudan Kusini yametoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuandaa mazingira ya ufikishaji misaada kwa waathirika wa vita vya ndani nchini humo.

Taarifa hiyo ya pamoja imetolewa na shirika la kimataifa la utoaji misaada la Oxfam na Kamati ya Kimataifa ya Uokozi kufuatia ripoti kadhaa zinazoeleza kuwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko nchini Sudan Kusini wameshindwa kutekeleza kazi ya kuwalinda raia na hujuma za vikosi vya serikali zikiwemo za ubakaji wanawake.

Inasemekana kuwa kikosi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini kina askari wapatao 12,000 ambao wamepewa mamlaka kamili ya kutumia silaha kwa ajili ya kulinda maisha ya raia wa nchi hiyo.

Askari wa Umoja wa Mataifa walioko nchini Sudan Kusini

Kazi nyengine ya askari hao ni kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia walioathiriwa na vita. Hii ni katika hali ambayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alitangaza siku ya Alkhamisi kuwa kutokana na kuwepo mazingira hatarishi, hali ya mambo ingali mbaya nchini Sudan Kusini. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amebainisha pia kuwa ahadi zilizotolewa kuhusu kupatikana amani, uadilifu na fursa katika taifa hilo jipya hazijatekelezwa.

Mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba, hivi karibuni umekumbwa na mapigano makali baina ya vikosi vya serikali na askari watiifu kwa Riek Machar, Makamu wa Rais na kiongozi wa waliokuwa waasi wa nchi hiyo; mapigano ambayo yamesababisha kuuawa watu zaidi ya 300.

Umoja wa Mataifa umetahadharisha pia kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia ambavyo vimeripotiwa kufanywa mjini Juba.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema, kesi 120 za ukatili wa kijinsia na ubakaji zimeripotiwa Sudan Kusini tangu yalipoanaza mapigano mapya baina pande mbili hasimu nchini humo yapata majuma matatu yaliyopita.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq

Farhan Haq ameongeza kuwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa wametoa ripoti zenye kutia wasiwasi mno kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia ukiwemo ubakaji na ubakaji wa kimakundi unaofanywa na askari waliovalia sare za jeshi dhidi ya raia katika mji mkuu wa nchi hiyo. 

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amefafanua kuwa askari wa kulinda amani wa umoja huo wameongeza operesheni za upigaji doria na kufanya jithada za kutoa ulinzi kwa wanawake mjini Juba na katika maeneo mengine ya Sudan Kusini.

Farhan Faq amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unazitaka pande zote nchini Sudan Kusini zihakikishe wahusika wa vitendo hivyo vya ukatili wanaadhibiwa haraka.

Itakumbukwa kuwa Riek Machar, akiwa kiongozi wa waasi na Rais Salva Kiir ambao ni mahasimu wawili wakuu katika vita vya ndani vya Sudan Kusini walisaini makubaliano ya amani mwezi Agosti mwaka uliopita wa 2015. Hata hivyo licha ya Machar kurudi mjini Juba na kushiriki kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa kufuatia makubaliano hayo, mapigano yamezuka upya  katika mji huo, hali iliyomfanya Makamu huyo wa Rais wa serikali hiyo ya pamoja auhame mji mkuu huo.

Rais Salva Kiir na Riek Machar, mahasimu wa kisiasa katika mgogoro wa Sudan Kusini

Kufuatia hatua ya Riek Machar kuondoka mjini Juba, Rais Salva Kiir amemteua Taban Deng Gai kuwa Makamu wake. Taban Deng Gai alikuwa kiongozi wa ujumbe wa waasi,waliokuwa waliokuwa chini ya Machar, katika mazungumzo ya amani ya nchi hiyo. 

Hayo yamejiri katika hali ambayo Machar alikuwa amemwandikia barua Rais Kiir kuwa amemvua Gai wadhifa alionao na kusisitiza kwamba atamteua mtu wa kushika nafasi yake baada ya yeye mwenyewe kurudi mjini Juba.

Hivi sasa mgogoro na mpasuko wa kisiasa nchini Sudan Kusini umezidi kuongezeka katika hali ambayo raia wanaokadiriwa kufikia milioni nne na laki nane,ambao ni karibu nusu ya watu wote wa nchi hiyo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) akitahadharisha kuwa hali ya kibinadamu nchini Sudan Kusini inatia wasiwasi.../