Niger: Kutimuliwa maajinabi kumefungua ukurasa mpya wa amani nchini
Balozi wa Niger mjini Tehran amesema lengo kuu la serikali mpya ya nchi yake ni kupata uhuru kamili.
Seydou Zetau Ali, Balozi wa Niger hapa nchini Iran amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press na kueleza kuwa, serikali mpya ya nchi yake inatoa kipaumbele kwa suala la kuhakikisha kuwa taifa hilo la Afrika Magharibi linakuwa na mamlaka kamili ya kujitawala.
Mwanadiplomasia huyo wa Niger ameeleza bayana kuwa, kuondolewa kwa vikosi vya kigeni kunaashiria mwanzo wa enzi mpya ya amani kwa nchi hiyo ya Kiafrika.
Amesema kufuatia mapinduzi ya Julai 2023, ambayo yalimuondoa madarakani Rais Mohammad Bazoum na kumuingiza uongozini Kanali Abdoulaye Tiani, Niger 'inajinyakulia' tena mamlaka yake.
Mabadiliko hayo muhimu hayalengi tu kurejesha uthabiti nchini humo kwa kupunguza uingiliaji kutoka nje, lakini pia kuhakikisha kwamba taifa hilo linaweza kujitegemea kusimamia rasilimali zake nyingi za asili, na hivyo kuunda upya mustakabali wake.
Baada ya kuvifukuza vikosi vya maajinabi na kuzipokonya leseni kampuni za Ulaya, serikali na Niger imekuwa ikisisitiza kuwa, kila nchi ina haki ya kuweka sheria za kusimamia mambo yake.