Afrika Kusini: Usitishaji vita Gaza sharti ulete amani ya kudumu
Rais wa Afrika Kusini amesema usitishaji wa mapigano katika Ukanda wa Gaza unapasa kuleta uadilifu na amani ya kudumu katika eneo hilo.
Pars Today ikinukuu shirika la habari la IRNA imeripoti kwamba, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amekaribisha usitishaji vita kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) na Israel na kuitaja kuwa hatua ya kimsingi ya kutatua mzozo wa kibinadamu huko Gaza.
Ameashiria migogoro katika maeneo mengine ya dunia, akisema: "Mizozo ya Ukraine, Sudan, Gaza imeigharimu pakubwa jamii ya mwanadamu katika maeneo mengine ya dunia."
Afrika Kusini ilikuwa taifa la kwanza kuiburuza Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kutokana na vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Gaza, ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 48,000, mbali na kuliacha eneo hilo kuwa magofu.
Pretoria imeapa kutoondoa kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya ICJ, licha ya vitisho, mashinikizo na kukatiwa misaada na utawala wa Donald Trump wa Marekani.
Kadhalika Rais wa Afrika Kusini amebainisha kuwa, zaidi ya watu bilioni 3.4 wanaishi katika nchi zinazokabiliwa na malimbikizi ya madeni, na kwa msingi huo, kuna haja ya kuongezwa juhudi za kutatua mgogoro huo wa madeni.