Shambulio la kigaidi kwenye msikiti nchini Niger laua makumi ya watu
(last modified Sat, 22 Mar 2025 07:01:46 GMT )
Mar 22, 2025 07:01 UTC
  • Shambulio la kigaidi kwenye msikiti nchini Niger laua makumi ya watu

Makumi ya watu wameuawa shahidi katika shambulio la kundi la kigaidi la ISIS kwenye msikiti mmoja kusini magharibi mwa Niger.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Niger imetangaza katika taarifa iliyosomwa kwenye Televisheni ya Taifa ya Niger (Tele Sahel) kwamba watu 44 wameuawa katika shambulio la magaidi wa ISIS kwenye msikiti wa kijiji cha Fonbita katika wilaya ya Kokorou kusini magharibi mwa Niger.

Habari hiyo imethibitishwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Niger, Mohamed Toumba na kwamba mauaji hayo yametokea wakati wanamgambo waliotambuliwa kuwa wanachama wa ISIS katika Sahara Kubwa (ISGS) walipovamia msikiti, wakiwalenga waumini.

Waziri Toumba amesema, majeruhi wanne kati ya 13 ambao walijeruhiwa katika shambulizi hilo, wako katika hali mbaya.

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Niger imelaani shambulio hilo na kusema ni "kitendo cha woga na kisicho cha kibinadamu" na kuahidi kuzidisha juhudi za kupambana na ugaidi katika eneo hilo.

Serikali ya Niger imetangaza saa 72 za maombolezo ya kitaifa kuanzia leo Jumamosi kuwaenzi wahanga wa shambulizi hilo la kigaidi.

Eneo la kusini-magharibi mwa Niger, hasa maeneo ya karibu na mipaka ya Mali na Burkina Faso, limeshuhudia ongezeko la ghasia katika miaka ya hivi karibuni, huku makundi kama ISGS yakitumia hali ukosefu wa amani kufanya mashambulizi dhidi ya vijiji na askari usalama.

Shambulio hilo linadhihirisha changamoto za kiusalama zinazolikabili taifa hilo la eneo la Sahel, licha ya juhudi zinazofanywa na serikali na Niamey na washirika wa kimataifa kukabiliana na uasi huo.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio hilo, ingawa Wizara ya Mambo ya Ndani inalituhumu kundi la ISGS linaloendesha shuli zake katika eneo hilo.