Guinea yatoa msamaha uliobua utata kwa kiongozi wa zamani wa kijeshi Dadis Camara
Mar 30, 2025 02:38 UTC
Katika uamuzi wa kutatanisha, kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Guinea, Jenerali Mamadi Doumbouya, ametoa msamaha wa rais kwa mtawala wa zamani wa kijeshi Moussa Dadis Camara.
Camara, aliyepatikana na hatia ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa alivyohusika katika mauaji ya 2009 yaliyofanyika mjini Conakry, amesamehewa kwa kilichoelezwa kuwa ni "sababu za kiafya." Uamuzi huo umetolewa kupitia tangazo lililotangazwa na televisheni ya taifa siku ya Ijumaa.
Amri hiyo iliyosomwa na msemaji wa ofisi ya rais Jenerali Amara Camara imesema, msamaha huo umetolewa kwa pendekezo la Waziri wa Sheria. Hata hivyo, hakukuwepo na dalili zozote zilizoashiria kuzorota kwa afya ya Camara, na hivyo kuibua mashaka juu ya sababu halisi iliyo nyuma ya uamuzi huo.
Camara, ambaye alitawala Guinea kuanzia mwaka 2008 hadi 2009, alihukumiwa Julai 2024 kwa kuhusika na ukandamizaji wa kikatili wa maandamano ya upinzani kwenye eneo la Grand Stade mjini Conakry.
Zaidi ya watu 150 waliuawa, na zaidi ya wanawake 100 walibakwa na vikosi vya usalama vilivyokuwa chini ya uongozi wake.
Kesi yake, iliyopewa msukumo na uchunguzi ulioidhinishwa na Umoja wa Mataifa, ilimpata kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi na hatia ya kushindwa kuzuia au kuwaadhibu wahusika wa ukatili huo.
Camara alikuwa kifungoni tangu aliporejea Guinea mwaka 2022 baada ya miaka 13 ya kuishi uhamishoni.
Uamuzi wa kutoa msamaha kwa kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi umezua wasiwasi kuhusu msimamo wa Guinea wa kusimamia haki na kuelezewa kama ishara ya mabadiliko katika mchakato wa mpito wa suala hilo chini ya uongozi wa Jenerali Doumbouya.../
Tags