UNHCR: Maelfu wamekimbia machafuko Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12484-unhcr_maelfu_wamekimbia_machafuko_sudan_kusini
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa maelfu ya watu wamekimbia machafuko na mapigano mapya yaliyozuka nchini Sudan Kusini huku kukiripotiwa matukio ya mauji ya umati, uporaji na watoto wadogo kushirikishwa vitani kwa nguvu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 02, 2016 21:53 UTC
  • UNHCR: Maelfu wamekimbia machafuko Sudan Kusini

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limetangaza kuwa maelfu ya watu wamekimbia machafuko na mapigano mapya yaliyozuka nchini Sudan Kusini huku kukiripotiwa matukio ya mauji ya umati, uporaji na watoto wadogo kushirikishwa vitani kwa nguvu.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa jana na shirika hilo la Umoja wa Mataifa, wengi kati ya wakimbizi hao wanaomiminika katika nchi jirani za Uganda, Ethiopia na Sudan wanaandamana na watoto wao wenye matatizo ya lishe duni ambao ni waathirika wa hali mbaya ya kibinadamu iliyochangiwa na uhaba wa chakula na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Melissa Fleming, msemaji wa UNHCR

Msemaji wa UNHCR Melissa Fleming amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva kwamba makundi yenye silaha yanayoendesha harakati zao katika sehemu mbalimbali za Sudan Kusini yanapora katika vijiji, yanaua raia na kuwalazimsiha wanaume vijana na watoto kujiunga na makundi hayo.

Wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Uganda

Amesema watu wapatao 60.000 wameikimbia nchi tangu machafuko yalipopamba moto, zaidi ya majuma matatu yaliyopita, wengi wao wakielekea nchini Uganda.

Afisa wa OCHA, Jens Laerke

Afisa wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya Kibinadamu (OCHA) Jens Laerke, amesema raia wengine milioni moja na laki sita wa Sudan Kusini ni wakimbizi ndani ya nchi yao.

Naye msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Fadela Chaib ameeleza kuwa mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu unaenea nchini humo huku kila siku zikiripotiwa kesi mpya 35 za wagonjwa wanaolazwa katika kaunti ya Juba.

Sudan Kusini ambayo ni taifa changa zaidi duniani imekumbwa na vita na machafuko ya zaidi ya miaka miwili yalichochewa na sababu za ukabila kati ya waungaji mkono wa Rais Salva Kiir na hasimu wake wa muda mrefu Riek Machar, mapiganio ambayo yamezusha hofu ya ukosefu wa amani kuenea katika sehemu kubwa ya eneo la Afrika Mashariki.

Wafuasi wa Machar wamesema watu wasiopungua tisa wameuawa katika mapigano ya karibuni mwishoni mwa juma katika barabara moja ya jimbo la Central Equatoria, eneo linalojumuisha pia mji mkuu wa nchi hiyo Juba.

Hata hivyo msemaji wa serikali Michael Makuei Lueth amezitoa maanani ripoti hizo na kusisitiza kuwa makubaliano ya amani yaliyovunjika hivi karibuni ambayo yalisainiwa mwaka uliopita yangali yako palepale. Akizungumza na waandishi wa habari hii leo Lueth amesema:"Watu wanapaswa waelewe kwamba makubaliano ya amani hayahusiani na Riek Machar".

Michael Makuei Lueth, msemaji wa serikali

Helikopta za jeshi la serikali zilionekana kupaa katika mji mkuu Juba  mwishoni mwa juma, lakini mitaa na barabara za mji mkuu wa Sudan Kusini zilionekana kuwa shwari hapo jana.