Waislamu Nigeria wawakumbuka Mashahidi wa Siku ya Quds
(last modified Mon, 12 May 2025 11:14:06 GMT )
May 12, 2025 11:14 UTC
  • Waislamu Nigeria wawakumbuka Mashahidi wa Siku ya Quds

Taasisi ya 'Wakfu wa Shuhada' ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imewakumbuka na kuwaenzi mashahidi 27 waliouawa na vikosi vya jeshi la nchi hiyo wakati wa maandamano ya amani ya Siku ya Quds ya 2025 huko Abuja, na kusisitiza kujitolea kwao kwa kadhia ya Palestina.

Auwal Darazo, mkuu wa Wakfu wa Shuhada katika Jimbo la Bauchi, alitoa wito kwa jamii ya Waislamu nchini Nigeria kuweka kando tofauti zao, kuungana na kuendeleza uungaji mkono wao kwa Wapalestina.

Sheikh Ahmad Yusuf Yashi, akimwakilisha Sheikh Ibrahim Zakzaky katika Jimbo la Bauchi, alisema Harakati ya Kiislamu ya Nigeria bado iko imara katika uungaji mkono wake kwa Palestina, licha ya ukandamizaji wa kila mwaka unaofanywa na serikali wakati wa maadhimisho ya Siku ya Quds, ambao husababisha maafa.

Picha za mashahidi zilionyeshwa wazi wakati wa hafla hiyo huko Bauchi. Waliozungumza kwenye maadhimisho hayo walisisitiza kuwa hakuna vitisho vya serikali ambavyo vitazuia uungaji mkono wao kwa Wapalestina.

Makumi ya watu walipoteza maisha nchini Nigeria huku vikosi vya usalama vikikabiliana kwa mabavu na maandamano ya amani ya Siku ya Quds ya mwaka huu 2025 huko Abuja na Kaduna.

Katika maandamano hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds yaliyofanyika nchini Nigeria kwa kushirikisha mamia ya Waislamu na wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo – kwa lengo la kuonyesha mshikamano na watu wa Palestina na kulaani uhalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel– maafisa wa polisi wa Nigeria walifyatua risasi dhidi ya waandamanaji na kuua, kujeruhi na kukamata makumi miongoni mwao.