TRA Tanzania kupita nyumba hadi nyumba kuchunguza upangishaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12709-tra_tanzania_kupita_nyumba_hadi_nyumba_kuchunguza_upangishaji
Katika hali ya kushangaza, Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA), imetangaza kuwa itaanza kutembelea nyumba hadi nyumba kuhakiki gharama za upangishaji kwa lengo la kukokotoa na kukusanya kodi sahihi ambazo zilikuwa hazifiki serikalini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 06, 2016 00:05 UTC
  • TRA Tanzania kupita nyumba hadi nyumba kuchunguza upangishaji

Katika hali ya kushangaza, Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA), imetangaza kuwa itaanza kutembelea nyumba hadi nyumba kuhakiki gharama za upangishaji kwa lengo la kukokotoa na kukusanya kodi sahihi ambazo zilikuwa hazifiki serikalini.

Aidha imewataka Watanzania kutunza kumbukumbu za mikataba yao ya upangaji ili itakapohitajika na maafisa wa mamlaka hiyo waweze kuwapatia. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati akielezea kuhusu makusanyo ya kodi kwa mwezi Julai mwaka huu, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema kuwa, hatua hiyo ni moja ya mikakati ya kuongeza ukusanyaji mapato kwa mamlaka hiyo nchini. Kwa mujibu wa Bwana Richard jumla ya Shilingi trilioni 1.055 ambazo ni sawa na asilimia 95.6 ya lengo la kukusanya Shilingi trilioni 1.103 iliyopangwa na serikali zilikusanywa na TRA ndani ya mwezi huo.

Richard Kayombo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA

Alisema na hapa ninamnukuu, “natoa wito kwa wapangaji na wapangishaji kujiepusha na aina yoyote ya udanganyifu katika suala zima la kodi halisi ya pango kwa kuwa inaweza kuwasababishia kushtakiwa endapo udanganyifu huo utabainika,” alisema Richard Kayombo. Kwa sasa, wapangaji wengi hawalipi kodi serikalini baada ya kupanga nyumba, na badala yake wamekuwa wakilipa fedha za pango kwa wamiliki wa nyumba ambao wengi wao pia hawalipi kodi serikalini zaidi ya kulipia kodi za majengo. Inaelezwa kuwa, wapangaji wengi wamekuwa wakilipishwa kodi ya pango kuanzia ya miezi sita hadi mwaka mmoja na kodi hizo zimekuwa zikitofautiana kutokana na hadhi ya nyumba, eneo ilipo, ukubwa wake na huduma ilizonazo kama maji na umeme.