ANC yapigwa mweleka katika mji mkuu Pretoria
Chama tawala nchini Afrika Kusini cha Congresi ya Taifa (ANC) kimepigwa mweleka wa kihistoria na chama cha upinzani cha Muungano wa Demokrasia (DA) katika uchaguzi wa mabaraza ya miji huko Tshwane ambayo yanahesabika kuwa makao makuu ya Pretoria mji mkuu wa uendeshaji.
Tume ya Uchaguzi ya Afrika Kusini imetangaza kuwa chama cha DA ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini humo kimeshinda asilimia 43 ya kura katika manispaa ya Tshwane. Chama tawala ANC kimeshinda asilimia 41 ya kura kulingana na matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na tume hiyo. Kushindwa chama cha ANC huko Pretoria kunaashiria kupungua pakubwa uungaji mkono wa wananchi kwa chama hicho ambacho kiliongoza mapambano dhidi ya mfumo wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini.
Jana chama tawala kilikubali matokeo ya uchaguzi wa mabaraza ya mji huko Port Elizabeth, mji ambao unahesabiwa kuwa ngome muhimu ya mchuano wa uchaguzi. Kushindwa ANC huko Port Elizabeth kumetathimiwa na weledi wa mambo kuwa pigo la udhalilishaji kwa chama tawala ANC katika manispaa hiyo ya mzee Nelson Mandela, mji ambao ulifahamika kwa historia yake ya kuwa kitovu cha harakati za mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi (Apartheid).