UN yaonya juu ya hali mbaya ya kibinaadamu nchini Sudan Kusini
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshusika na Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu na Misaada ya Dharura ameonya juu ya ukosefu wa makazi na ukame huko nchini Sudan Kusini.
Stephen O'Brien amesema kuwa hali mbaya Sudan Kusini ilikuwa ya kiwango kikubwa mwaka jana 2015 na kwamba hivi sasa tatizo la ukosefu wa makazi na ukame vimeenea nchi nzima na kuifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi. Amesema kuwa, mwezi Julai pekee uliopita jumla ya watu elfu 70 raia wa Sudan Kusini walivuka mpaka wa nchi hiyo na kuingia Uganda. Kwa mujibu wa Stephen O'Brien, karibu watu milioni nne na laki nane wanakabiliwa na njaa kali na ukame. Ameongeza kuwa watoto laki mbili na nusu wamekumbwa na lishe duni ya kupindukia.
Kadhalika Mratibu huyo wa Masuala ya Kibinaadamu na Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa ametoa shukurani kwa jamii ya kimataifa kwa kudhamini msaada wa zaidi ya nusu bilioni dola za Marekani na kusema kuwa, hata hivyo bado kuna uhaba wa kiasi cha dola milioni 700 kwa ajili ya kudhamini mahitaji ya kibinaadamu nchini humo. Mapigano makali katika mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba yaliibuka mwanzoni mwa mwezi jana Julai kati ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir, na wale wanaomuunga mkono makamu wa zamani wa rais wa taifa hilo, Riek Machar. Katika mapigano hayo watu wasiopungua 300 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.