Wafanyakazi wa Shirika la Umeme Afrika Kusini waitisha mgomo
Wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini Afrika Kusini wametoa wito wa kuendeleza mgomo wa wafanyakazi wote wa shirika hilo kwa lengo la kushinikiza kuongezewa mshahara wao.
Livhuwani Mammburu, msemaji wa Umoja wa Wafanyakazi nchini humo (NUM) ametangaza kufanyika maandamano na mgomo wa maelfu ya wafanyakazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme nchini Afrika Kusini (ESKOM) katika mkoa wa Mpumalanga mashariki mwa nchi hiyo na ametishia kuendelezwa mgomo huo hadi matakwa yao yatakapotekelezwa.
Mammburu amesisitizia kuendelezwa mgomo wa wafanyakazi wa sekta hiyo ya umeme nchini kwa lengo la kutekelezwa matakwa yao ya kimsingi ambayo ni kupandishiwa mshahara. Karibu wafanyakazi elfu 15 wa shirika hilo la umeme wanashiriki kwa namna tofauti maandamano hayo nchi nzima.
Wafanyakazi hao wanalitaka shirika hilo kuwaongezea asilimia 10 ya mishahara yao wakati shirika hilo (ESKOM) limeahidi kuongeza asilimia saba hadi tisa pekee ya mishahara ya wafanyakazi wake.
Kadhalika Jumuiya ya Wafanyakazi ya Afrika Kusini inalituhumu shirika hilo kuwa linatoa mshahara mnono kwa wafanyakazi wazungu na mshahara kiduchu kwa wafanyakazi wazalendo weusi.