Kupungua ushawishi wa chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini
Matokeo ya kura za uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Afrika Kusini zilizohesabiwa hadi sasa yanaonesha kupungua ushawishi wa chama tawala cha ANC nchini humo.
Kamisheni ya uchaguzi nchini Afrika Kusini inasema kura zilizohesabiwa za uchaguzi wa mabaraza ya miji uliofanyika hivi karibuni nchini humo zinaonyesha kwamba katika miji mikubwa, chama cha upinzani cha Democratic Alliance (DA) kimepata asilimia 46/65 ya kura, huku chama tawala cha African National Congress (ANC) kikipata asilimia 40/99, suala linaloonyesha kupungua ushawishi wa chama hicho tawala ndani ya taifa hilo.
Tangu chama cha ANC kilipojipatia ushindi katika uchaguzi wa kwanza Aprili 1994 kwa uongozi wa Mzee Nelson Mandela, kimekuwa kikipata ushindi wa takribani asilimia 60 katika akthari ya chaguzi za nchi hiyo. Chama hicho kilijipatia asilimia 50 ya kura katika miji mikubwa katika uchaguzi wa mwaka 2011. Pigo kubwa la chama tawala katika uchaguzi wa mara hii wa mabaraza ya miji ni kupigwa mweleka na upinzani katika mji wa Port Elizabeth.
Mji huo ulikuwa kitovu cha harakati za mzee Nelson Mandela na kubwaga ANC na upinzani katika mji huo kunahesabiwa kuwa ni pigo kubwa mno kwa chama hicho tawala. Kwa kuzingatia umaarufu wa vyama vingine vya siasa na pia kuendelea kuongezeka ushawishi wa vyama hivyo hususan katika uchaguzi wa mara hii, kunatazamiwa kujitokeza mabadiliko katika nafasi za kiuongozi nchini Afrika Kusini.
Baadhi ya waungaji mkono wa chama tawala wanaamini kuwa, kueneza hisia ya kukata tamaa baina ya wananchi kulikofanywa na baadhi ya vyombo vya habari vya Magharibi ndiyo iliyokuwa sababu ya kushadidi mivutano ndani ya chama cha ANC na kupungua uungaji mkono wa watu kwa Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo.
Katika mazingira haya, duru za kisiasa zimeutaja uchaguzi wa mara hii wa mabaraza ya miji nchini Afrika Kusini kuwa ni sawa na kura ya maoni ya kuangalia mapenzi na uungaji mkono wa wananchi wa nchi hiyo kwa chama tawala cha ANC.
Mdororo wa kiuchumi na asilimia 27 ya kiwango cha ukosefu wa ajira sambamba na mafaili meusi ya ufisadi ya viongozi wa chama cha ANC akiwemo Rais Zuma, ni mambo yanayotajwa na weledi wa mambo kuwa, yamekuwa na taathira kubwa ya kupendwa vyama vya upinzani kikiwemo cha Democratic Alliance DA.
Baada ya kufanyika uchaguzi huo, sasa vyama vya kisiasa vimo mbioni kushirikiana na asasi za serikali kwa shabaha ya kutekeleza miradi mbalimbali ya miji.
Ripoti zinaonesha kuwa, chama cha upinzani cha Democratic Alliance DA kimeanza kufanya mazungumzo na asasi za serikali na vyama vingine vya kisiasa kwa lengo la kutekeleza miradi ya miji iliyopasishwa na serikali.
Chama cha mrengo wa kushoto nchini Afrika Kusini nacho kimeanza kujikurubisha na vyama vingine amilifu nchini humo. Rais Jacob Zuma amesema kuwa, kuendeshwa vizuri uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini humo ni ithbati tosha ya ukomavu wa kidemokrasia nchini humo.
Akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo, Rais Zuma alisema, uchaguzi huo umeshuhudia vuta nikuvute na ushindani mkali na vyama pinzani vimefanya kila viwezalo vikielezea mitazamo yao kwa hamasa kubwa ili viweze kuibuka na ushindi.