HRW yaitaka Misri ichunguze mauaji ya mamia ya watu 2013
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13303-hrw_yaitaka_misri_ichunguze_mauaji_ya_mamia_ya_watu_2013
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelitaka bunge la Misri lianzishe uchunguzi huru na usioegemea upande wowote juu ya mauaji ya mamia ya waandamanaji mnamo Julai mwaka 2013.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 15, 2016 03:36 UTC
  • HRW yaitaka Misri ichunguze mauaji ya mamia ya watu 2013

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limelitaka bunge la Misri lianzishe uchunguzi huru na usioegemea upande wowote juu ya mauaji ya mamia ya waandamanaji mnamo Julai mwaka 2013.

Taarifa ya Human Rights Watch imewataka wabunge wa Misri kupasisha sheria itakayoruhusu kufanyika uchunguzi huru juu ya mauaji yaliyofanywa na maafisa usalama dhidi ya waandamanaji, ili kuwafikisha mbele ya sheria waliotenda jinai hizo sambamba na kuzifidia familia za wahanga wa mauaji na ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji, wakati wa mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Rais wa sasa Abdel Fattah el-Sisi dhidi ya Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia na misingi ya demokrasia Muhammad Morsi.

Maandamano ya amani ya wananchi wa Misri

Sarah Leah Whitson, ofisa wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu amesema kuwa, iwapo serikali ya sasa inataka kupata ridhaa ya maelfu ya wananchi wa Misri ambao wamepitia kipindi kigumu katika muda wa miaka mitatu iliyopita, sharti iwawajibishe wahusika wa jinai hizo.

Rais wa zamani wa Misri, Muhammad Morsi

Kwa mujibu wa HRW, watu kati 800 na 1000 waliuawa katika maandamano hayo, ambayo shirika hilo la kutetea haki za binadamu linasema ni jinai dhidi ya binadamu.

Itakumbukwa kuwa, baada ya kuondolewa madarakani Muhammad Morsi, polisi ya Misri iliwatia mbaroni maelfu ya wafuasi wa rais huyo huku baadhi yao wakihukumiwa adhabu ya kifo.