Mtetezi wa haki za binadamu Kenya atangaza mshikamano na watu wa Iran
Mwanaharakati maarufu wa haki za binadamu nchini Kenya, Shakira Wafula, ametangaza mshikamano wake na watu wa Iran na Palestina, akitoa ujumbe wa imani na matumaini.
Kwa mujibu wa Idara ya Mahusiano ya Umma ya Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu, “Shakira Wafula,” mtetezi wa haki za binadamu kutoka Kenya, amesema:
"Nikiwa mtetezi wa haki za binadamu kutoka Kenya, napenda kuwasilisha ujumbe wangu wa mshikamano kwa ndugu na dada zangu wa Iran, Palestina, na maeneo yote ambako watu wanakabiliwa na dhuluma na mateso.
Ameongeza: Tunasimama pamoja nanyi, tunamuomba Mwenyezi Mungu awawatie moyo, nguvu na ustahimilivu ili mshinde katika safari hii ngumu.
Mtetezi huyu wa haki za binadamu amesisitiza: Tunapinga vitendo vyote vya udhalilishaji na uonevu, na hatutaruhusu maangamizi na mateso ya watu, haswa huko Gaza, kuendelea au vita kuenea hadi nchi nyingine ikiwemo Iran.
Amesema: Leo hii, dhamiri zilizo hai duniani kote ziko upande wenu. Tunaomba haki, na tunatumai amani, usalama na heshima ya binadamu vitadumu kwa watu wote."
Kumefanyika mijimuiko kadhaa nchini Kenya na maeneo mbali mbali barani Afrika kulaani hujuma ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya Iran.
Hivi karibuni pia Wananchi wa Afrika Kusini walifanya maandamano na mikusanyiko mikubwa wakionyesha uungaji mkono wao kwa Iran kufuatia uvamizi wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Watunisia pia wamefanya maandamano ya kuiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kukosoa kauli ya Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ambayo haikulaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya taifa la Iran.
Nchini Nigeria maelfu ya Waislamu nchini Nigeria waliandamana hivi karibuni katika mji wa Kano, ulioko kaskazini mwa nchi hiyo, wakilaani mashambulizi ya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kutangaza wazi uungaji mkono wao kwa taifa hilo.
Washiriki wa maandamano hayo pia walionesha mshikamano wao na Iran pamoja na umma mpana wa Waislamu. Baadhi ya waandamanaji walisema maandamano hayo ni ishara ya umoja na Iran, na pia ni sauti ya kupinga uingiliaji wa mataifa ya Magharibi katika masuala ya Asia Magharibi. Katika mitandao ya kijamii kote barani Afrika, aghalabu ya watu wameonysha mshikamano na Iran huku wakilaani vita dhidi ya nchi hii vinavyoendeshwa na Marekani na Israel.