Afrika Kusini yasisitiza mapambano dhidi ya ugaidi
Rais wa Afrika Kusini amesisitiza kuunga mkono juhudi za mapambano dhidi ya ugaidi.
Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za kieneo na kimataifa za kupambana na ugaidi katika miundo yake yote. Rais Zuma ameyasema hayo baada ya kutokea shambulio Jumamosi katika mji wa Gaziantep kusini mashariki mwa Uturuki na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 50 na kujeruhi makumi ya wengine. Itakumbukwa kuwa mtoto aliyekuwa na umri kati ya miaka 12 na 14 Jumamosi iliyopita alijilipua kwenye sherehe ya harusi katika mji wa Gaziantep Uturuki na kuua watu zaidi ya 50 waliokuwa katika marasimu hayo. Rais Reecep Tayyep Erdogan wa Uturuki amelituhumu kundi la kigaidi la Daesh kuwa limetekeleza shambulio hilo.
Rais wa Afrika Kusini ametoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Uturuki kufuatia shambulio hilo na kusisitiza kuwa serikali ya Pretoria inalaani shambulio hilo la umwagaji damu dhidi ya raia. Rais Zuma ameongeza kuwa Afrika Kusini imejiunga na jamii ya kimataifa kulaani suala la ugaidi. Zuma amesema wananchi wa Afrika Kusini pia wanatoa mkono wa pole kwa serikali na wananchi wa Uturuki hususan familia za wahanga wa shambulio lililotekelezwa katika mji wa Gaziantep nchini Uturuki. Wananchi wa Afrika Kusini wamesema wanataraji kuwa majeruhi wa shambulio hilo watapata nafuu haraka iwezekanavyo.