TLP: Serikali ya SMZ ikifungie ruzuku chama cha CUF hadi kijirekebishe
Chama cha Tanzania Labour Party (TLP) nchini humo, kimemuandikia barua Rais wa Mapinduzi wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na kumtaka kuanzia sasa amtenge Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kwa kutomualika kwenye shughuli zozote za kitaifa.
Kwa Mujibu wa chama hicho, mwenendo huo wa kumtenga Maalim Seif unatakiwa uendelee hadi pale atakapojirekebisha na kuitambua rasmi serikali iliyopo madarakani visiwani Zanzibar.
Aidha, chama hicho kinachoongozwa na Augustino Lyatonga Mrema, kimeenda mbali zaidi na kudai kuwa, kwa kuwa CUF inasema kwamba haiitambui serikali ya chama tawala CCM, basi ruzuku kwa chama hicho inatakiwa pia isitishwe kuanzia sasa hadi pale chama hicho kitakapoitambua rasmi serikali hiyo na kuacha kuhamasisha wananchi waache kulipa kodi. Hatua hiyo imekuja kufuatia hivi karibuni Maalim Seif ambaye pia alikuwa makamu wa kwanza wa rais kwenye serikali ya Umoja wa kitaifa Zanzibar (SUK), kususia kumpa mkono Rais Shein, wakati wa maziko ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, marehemu Mzee Aboud Jumbe, kitendo ambacho kilitafsiriwa na weledi wa mambo kuwa kilimdhalilisha rais huyo. Katika barua ya chama cha TLP iliyosainiwa na mwenyekiti wake, Augustine Mrema ilisema chama hicho kimesikitishwa sana na kitendo hicho.
Chama cha Mrema ambacho kimekuwa muitifaki mkubwa wa chama tawala CCM tangu Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania alipompatia wadhifa serikalini, kimeongeza kuwa, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa marudio uliosusiwa na chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif amekuwa akileta chokochoko na uchochezi dhidi ya serikali ya Zanzibar akidai kwamba haitambui na kuwataka wananchi wa Zanzibar wasilipe kodi kwa serikali.