Africa CDC: Ni mapema mno kutangaza mripuko wa Ebola umedhibitiwa DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141194-africa_cdc_ni_mapema_mno_kutangaza_mripuko_wa_ebola_umedhibitiwa_drc
Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) vimetangaza kuwa bado ni mapema mno kusema kwamba mripuko wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umedhibitiwa, licha ya kuweko dalili za kupungua sana ugonjwa huo katika wiki za hivi karibuni.
(last modified 2026-09-04T10:42:41+00:00 )
Sep 04, 2026 10:38 UTC
  • Africa CDC: Ni mapema mno kutangaza mripuko wa Ebola umedhibitiwa DRC

Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (Africa CDC) vimetangaza kuwa bado ni mapema mno kusema kwamba mripuko wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umedhibitiwa, licha ya kuweko dalili za kupungua sana ugonjwa huo katika wiki za hivi karibuni.

"Bado ni mapema kusema kwamba tumedhibiti mripuko mzima," afisa wa Africa CDC, Wessam Mankoula amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya mtandao, akibainisha kuwa mripuko huo "bado una sura ya kubadilika."

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni iliyochapishwa jana Alkhamisi, serikali ya DRC ilikuwa imerekodi kesi 6,250 zilizothibitishwa na vifo 3,039 kufikia Septemba 1, huku kiwango cha vifo kikiwa ni asilimia 48.6. Wagonjwa 1,439 wamepona. Mripuko huo umeathiri maeneo 60 ya afya katika majimbo sita ya DRC.

Maambukizi yamekatika kwenye maeneo manne ya afya baada ya kutoripotiwa kesi mpya kwa zaidi ya siku 42, huku maeneo mengine matano yakiwa katika "awamu ya udhibiti", ambayo yameshapitisha kati ya siku 21 na 42 bila ya kuripotiwa kesi yoyote mpya. "Hata hivyo, maambukizi yanaendelea katika maeneo 51 ya afya," amesema Mankoula.

"Kwa wiki mbili zilizopita, tunaona kupungua idadi ya kesi za ugonjwa huu; tumekaribia kufikia awamu ya uwanda wa juu," Mankoula alisema, akionya kwamba "ni mapema sana kusema tutaendelea kushuhudia kupungua mripuko huu."

Mripuko wa hivi sasa ulitangazwa mwezi Mei, na tangu wakati huo umekuwa ni janga kubwa na hatari zaidi la Ebola kuwahi kurekodiwa DRC na la pili kwa ukubwa duniani, baada ya lile janga kubwa la Ebola lililozikumba nchi za magharibi mwa Afrika katika miaka ya 2014-2016.

Mankoula pia amebainisha kuwa ingawa Uganda hivi karibuni ilitangaza kuisha mripuko wa Ebola, lakini kuendelea maambukizi katika majimbo ya mashariki mwa DRC yanayopakana na Uganda kunaleta hatari ya kurejea ugonjwa huo.