Umoja wa Mataifa wakataa kushambuliwa Daesh Libya
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema kuwa, huenda hivi sasa usiwe wakati mwafaka wa kufanya operesheni za kijeshi dhidi ya magaidi wa Daesh nchini Libya.
Gazeti la Ra'yul Yaum limemnukuu Martin Kobler, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kadhia ya Libya akitoa matamshi hayo ya kutatanisha na kudai kuwa, kama hivi sasa kutaanza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh, basi kuna uwezekano suala hilo likavuruga juhudi za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.
Gazeti hilo limekumbusha kuwa, mwezi Disemba mwaka jana, makundi hasimu nchini Libya yalifikia makubaliano yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, hata hivyo Baraza la Mawaziri la serikali hiyo halijapasishwa na bunge la nchi hiyo hadi hivi sasa.
Amesema, mashambulizi ya anga pekee hayatoshi kukabiliana na kundi la Daesh, bali kuna wajibu wa kufanyika operesheni za kijeshi za nchi kavu sambamba na mashambulizi ya anga na hilo kwa mtazamo wake haliwezekani kwa hivi sasa. Magaidi wa Daesh wanashikilia miji na vijiji kadhaa nchini Libya hususan mji wa Sirte.