UKUTA watangaza kuakhirisha maandamano ya kesho Tanzania
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14359-ukuta_watangaza_kuakhirisha_maandamano_ya_kesho_tanzania
Muungano wa vyama vya upinzani nchini Tanzania umeahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika kesho.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Aug 31, 2016 09:42 UTC
  • UKUTA watangaza kuakhirisha maandamano ya kesho Tanzania

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Tanzania umeahirisha maandamano ya kitaifa ambayo yalikuwa yamepangiwa kufanyika kesho.

Viongozi wa upinzani, akiwemo Edward Lowassa wa Chadema leo wametangaza hatua hiyo kwenye kikao na wanahabari jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wamesema kuwa, wameahirisha maandamano hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja baada ya kusikia ombi la viongozi wa kidini na wadau wengine waliowaomba kukumbatia na kuyapa muda mazungumzo.

Viongozi wa chama hicho walikuwa wameitisha maandamano na mikutano ya kisiasa Septemba Mosi kupinga walichosema kuwa ni ukandamizaji unaoendelezwa na serikali. Muungano huo wa wapinzani uliokuwa umepanga kufanya maandamano hayo hapo kesho unajulikana kwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA).

Baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mwishoni mwa mwezi Julai, viongozi walisema: "Yapo Matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na kukandamiza demokrasia na misingi ikipuuzwa na kudharauliwa."

Freeman Mbowe, Mwenyekiti Taifa wa chama cha upinzani cha Chadema

"Si nia ya Chadema kugombana na Serikali bali ni kazi ya Chama Pinzani kuisaidia Serikali iongoze kwa kufuata misingi ya Katiba," chama hicho kilisema.

Ikumbukwe kuwa vyombo vya usalama nchini Tanzania vilikuwa vimeyapiga marufuku maandamano hayo ya kesho na kusisitiza kwamba, itawachukulia hatua wale wote watakaoshiriki maandamano hayo.

Siku chache zilizopita serikali ya Tanzania ilitangaza kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa, ya hadhara na ya ukumbini.

Baadhi ya viongozi wa upinzani nchini humo wamekamatwa na kuzuiliwa kwa muda baada ya kukamatwa wakifanya mikutano ya kisiasa ya ndani.