Waziri Mkuu wa Libya: Vita dhidi ya Daesh vitaendelea
-
Fayez al-Sarraj, Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya
Waziri Mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ametembelea mji wa Sirte, uliokuwa ngome kuu ya genge la kigaidi la Daesh na kusema kuwa, mapambano dhidi ya kundi hilo yataendelea hadi kulimaliza kabisa.
Televiesheni ya Rusia al Yaum imemnukuu Fayez al-Sarraj akisema hayo leo na kuongeza kuwa, serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inawaunga mkono na kuwasaidia kwa kila hali askari walioko mstari wa mbele katika kupambana na kundi la kigaidi la Daesh na inawadhaminia mahitaji yao yote kama vile silaha, zana za kivita na matibatu.
Kwa upande wake, Muhammad al Ghasri, msemaji wa opereshenei ya "al-Bunyan al-Marsoos" amesema kuwa, askari wa Libya wamepata mafanikio makubwa katika operesheni za kijeshi katika eneo la mwisho linalodhibitiwa na Daesh huko Sirte na kuwasababishia hasara kubwa magaidi hao.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, askari wa serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wamepata ushindi muhimu katika mapambano yao na magaidi ya Daesh huko Sirte.
Kwa muda sasa askari wanaoiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya wamekuwa wakipambana na wanamgambo wa Daesh ambao walitumia mwanya wa kukosekana serikali kuu yenye nguvu nchini Libya baada ya kupinduliwa Kanali Muammar Gaddafi; kujipenyeza na kuteka baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ukiwemo mji wa Sirte ambao waliufanya kuwa ngome na makao yao makuu.