Uchaguzi wa Somalia kufanyika mwezi Julai mwaka huu
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Somalia amesema, viongozi wa baadhi ya majimbo nchini humo wamekubaliana na pendekezo la serikali kuu la kufanyika uchaguzi mwezi Julai mwaka huu.
Michael Keating, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amesema, kuendelea kuungwa mkono pendekezo la kufanyika uchaguzi mwaka huu kunaonyesha utashi wa Wasomali wa kufikia demokrasia kamili.
Mwanadiplomasia huyo wa UN amesema, usalama wa Somalia unategemea utulivu wa kisiasa na kwamba, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa wakati na kwa kadiri itakavyowezekana, itakuwa ni kwa maslahi ya taifa hilo na nchi majirani.
Serikali za majimbo nchini Somalia zinataka zoezi la uchaguzi liwashirikishe watu wote na viongozi wa mashinani wawe na nafasi ya kutoa maamuzi muhimu kwenye zoezi hilo.
Rais wa hivi sasa wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud ametangaza nia yake ya kuwania urais nchini humo. Spika Sharif Hassan Sheikh Aden pia anatarajiwa kuwania nafasi hiyo.