Iran na Tanzania kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia kuimarisha uhusiano wa kiutamaduni na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hayo yamesema na Mkuu wa Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu la Iran, (ICRO) Bw. Abudhar Ibrahim Turkman leo Jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo wa Tanzania Mhe. Nape Moses Nnauye. Katika kikao hicho Bw. Turkman amesema kuna nukta nyingi za pamoja za kiutamaduni baina ya Iran na Tanzania na jambo hilo limeandaa uwanja wa kuimarisha ushirikiano baina ya nchi mbili. Aidha amesisitiza kuwa, Wairani wameacha athari za kudumu za kiutamaduni nchini Tanzania.
Ibrahimi Turkman ametoa wito wa kutekelezwa makubaliano ya kiutamaduni baina ya Iran na Tanzania sambamba na kufanyika wiki ya utamaduni ya nchi mbili katika miji ya Dar es Salaam, Kilwa, Tehran na Shiraz.
Kwa upande wake, Waziri Nnauye alisema kuwa amekubaliana na wazo la kuanzishwa kwa wiki ya utamaduni kati ya Tanzania na Iran na kwamba ni fursa pekee ya kujifunza kutoka kwa Wairani namna ya kukuza, kulinda na kuuendeleza utamaduni wa Mtanzania.
“Utamaduni ni silaha ya upendo na nimefurahia wazo la kuanzisha Wiki ya Utamaduni na tuko tayari kujifunza kutoka kwenu na hakika tumelipokea na tunaamini fursa hii italeta mafanikio makubwa katika sekta hii”, alisema Mhe. Nnauye.
Aidha ameashiria uzoefu wa Iran katika sekta ya vyombo vya habari katika kukabiliana na propaganda chafu dhidi ya Iran inayoenezwa na baadhi ya nchi za Magharibi na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kutumia vyombo vya habari na simena na kuwavutia wengi na hivyo Tanzania nayo inataka kufaidika na uzoefu huu."
Katika kikao hicho, pande mbili zimejadili pia njia za kuunda tume ya pamoja ya utamaduni baina ya Iran na Tanzania.