Benki ya Dunia: Uchumi wa Tanzania, Rwanda unastawi kwa wastani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16366-benki_ya_dunia_uchumi_wa_tanzania_rwanda_unastawi_kwa_wastani
Benki ya Dunia imetoa ripoti ya ustawi wa uchumi wa Afrika ambapo nchi za Afrika Mashariki za Tanzania na Rwanda zinaonekana kuwa na uchumi wenye kustawi kwa wastani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 30, 2016 03:33 UTC
  • Benki ya Dunia: Uchumi wa Tanzania, Rwanda unastawi kwa wastani

Benki ya Dunia imetoa ripoti ya ustawi wa uchumi wa Afrika ambapo nchi za Afrika Mashariki za Tanzania na Rwanda zinaonekana kuwa na uchumi wenye kustawi kwa wastani.

Ripoti mpya ya Benki ya dunia itolewayo mara mbili kwa mwaka, Africa's Pulse , inaonyesha kuwa mwelekeo wa ukuaji uchumi barani Afrika unatarajiwa kudorora zaidi na kuwa asilimia moja nukta sita mwaka huu ikilinganishwa na asilimia tatu mwaka jana.

Ripoti hiyo hata hivyo imebainisha kuwa, mwelekeo wa ukuaji unatofautiana ambapo baadhi ya nchi ustawi umedorora huku nyingine uchumi unakua. Kwa mfano Rwanda, Tanzania na Ethiopia zimetajwa kuwa nchi zenye ustawi wa wastani ambao ni zaidi ya asilimia sita kwa mwaka, huku Cote d'Ivoire na Senegal zikiongoza kwa kasi ya ustawi barani Afrika.

Zao la ngano: Benki ya dunia imesisitiza umuhimu wa kilimo

Mchumi Mkuu wa Benki ya dunia kuhusu Afrika Albert Zeufack amesema chanzo cha kukwama ustawi wa uchumi ni kudorora kwa bei za bidhaa ikiwemo mafuta, hali ngumu ya kifedha na sera za uchumi zisizo makini.

Benki ya Dunia inasema mwelekeo ni kupanua wigo wa bidhaa zinazouzwa pamoja na kuboresha sekta ya kilimo hasa kwa wakulima wadogo wadogo ili kuinua vipato vyao na kupunguza umaskini.