Mjumbe wa Machar: IGAD inachochea machafuko S/Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16660-mjumbe_wa_machar_igad_inachochea_machafuko_s_kusini
Mpambe wa karibu wa Riek Machar, makamu wa zamani wa rais wa Sudan Kusini ameielekezea kidole cha lawala Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD kutokana na machafuko na mapigano yanayoshudiwa katika nchi hiyo changa zaidi duniani.
(last modified 2026-02-22T02:21:18+00:00 )
Oct 04, 2016 08:06 UTC
  • Mjumbe wa Machar: IGAD inachochea machafuko S/Kusini

Mpambe wa karibu wa Riek Machar, makamu wa zamani wa rais wa Sudan Kusini ameielekezea kidole cha lawala Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD kutokana na machafuko na mapigano yanayoshudiwa katika nchi hiyo changa zaidi duniani.

Katika mahojiano na jarida la Africa Review, Naibu Mjumbe wa Sudan Kusini nchini Tanzania, Peter Oyoyo Kleto, ambaye ni mtu wa karibu na Machar amesema jumuiya hiyo ya kieneo ilimlazimisha Dakta Machar arejee Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini pasina kumuandalia usalama na ulinzi wa kutosha kwa mujibu wa makubaliano ya amani. Kleto amesema IGAD ilimshurutisha Machar aelekee Juba bila askari na walinzi wa kutosha mbali na kumuagiza abebe silaha nyepesi huku akisisitiza kwamba, Machar aliponea chupuchupu na kwa 'Rehema ya Mungu' katika makabiliano makali ya Julai, kati ya askari wanaomuunga mkono na waitifaki wa Rais Salva Kiir mjini Juba.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Mwishoni mwa mwezi uliopita, makamu huyo wa zamani wa rais nchini Sudan Kusini alisema kuwa makubaliano ya amani na serikali ya Rais Salva Kiir hayana itibari yoyote na hivyo amewataka wafuasi wake kuanzisha vita upya. Machar aliyasema hayo akiwa Khartoum, mji mkuu wa Sudan ambako alikimbilia baada ya kuibuka machafuko ya mwezi Julai mwaka huu mjini Juba mji mkuu wa Sudan Kusini.

Wakimbizi wa Sudan Kusini nchini Uganda

Mvutano wa kisiasa baina ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka na Riek Machar wa kabila la Nuer, ulianza tangu miaka mitatu iliyopita na kusababisha vita vya ndani vilivyopelekea maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.