Al-Azhar yasisitiza ulazima wa kukabiliana na ugaidi
Sheikh Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al-Azhar nchini Misri amesisitizia ulazima wa kukabiliana na ugaidi.
Sheikh Ahmad At-Tayyib ametoa wito huo leo katika kikao maalumu kilichofanyika nchini Uswisi ambapo mbali na kutilia mkazo udharura wa kukabiliana na ugaidi ameeleza kuwa ugaidi umeusaliti Uislamu na dini nyingine za mbinguni.
Sheikh Mkuu wa Al-Azhar amebainisha kuwa dini na vitendo vya kigaidi ni vitu vyenye kugongana na akaongeza kwamba, baadhi ya watu wanataka kuuhusisha ugaidi na Uislamu ilhali viwili hivyo haviwezi katu kujumuika pamoja.
Sheikh Ahmad At-Tayyib amesema, makundi ya kigaidi yanatenda jinai dhidi ya binadamu kwa jina la Uislamu; na vitendo vyao hivyo ni usaliti wa wazi kwa Uislamu wa asili.
Mbali na kutangaza utayari wa Al-Azhar wa kushirikiana na Shura ya Wanahekima wa Kiislamu ambayo inatazamiwa kufanya kongamano maalumu mnamo mwezi huu mjini Abu Dhabi katika Umoja wa Falme wa Kiarabu (UAE),Sheih Ahmad At-Tayyib ameeleza kuwa kikao cha wanahekima na wanafikra wa nchi za Mashariki na Magharibi kilichopangwa kufanyika mwakani nchini Misri na kuhudhuriwa pia na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis wa Kwanza kitakuwa na matunda yenye faida kubwa kwa walimwengu.../