Rais wa Sudan Kusini akanusha uvumi kuwa ameuawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17305-rais_wa_sudan_kusini_akanusha_uvumi_kuwa_ameuawa
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amelazimika kujitokeza hadharani kukanusha uvumi ulioenea nchini humo kwamba ameuawa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 13, 2016 04:20 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini akanusha uvumi kuwa ameuawa

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amelazimika kujitokeza hadharani kukanusha uvumi ulioenea nchini humo kwamba ameuawa.

Habari zinasema kuwa, Rais Kiir alizunguka mjini Juba akiwa kwenye msafara uliowaleta pamoja maafisa wa ngazi za juu wa serikali ya nchi hiyo akiwemo Jenerali Paul Malong, kamanda mkuu wa vikosi vya majeshi na Michael Makuei, Waziri wa Habari na Mawasiliano wa nchi hiyo changa zaidi ya Kiafrika.

Jenerali Michael Chianyjiek, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo amesema vyombo vya usalama vitamtia mbaroni mtu yeyote atakayeeneza uvumi kuwa Rais Salva Kiir ameuawa. Taharuki ilitanda nchini Sudan Kusini kuanzia Jumanne usiku baada ya kusambaa habari za tetesi kuwa Rais wa Sudan Kusini ameaga dunia.

Riek Machar, kiongozi wa waasi Sudan Kusini

Hii ni katika hali ambayo, Riek Machar, kiongozi wa waasi wa nchi hiyo ambaye alikimbilia Khartoum baada ya mapigano makali yaliyotokea katika mji mkuu Juba Julai mwaka huu baina ya wafuasi wake na jeshi la serikali ya Rais Salva Kiir, ameondoka nchini Sudan na kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake.

Mamia ya watu waliuawa na mamia ya maelfu ya wengine kuuhama mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba na kukimbilia maeneo mengine baada ya kuzuka mapigano kuanzia tarehe 8 hadi 11 mwezi Julai mwaka huu baina ya askari watiifu kwa Rais Salva Kiir na wapiganaji wanaomuunga mkono Riek Machar.