Mgogoro wa kisiasa waongezeka nchini Libya
Taasisi ya kulinda usalama iliyoko chini ya amri ya baraza la uongozi wa Libya imetangaza kujitenga na baraza hilo.
Shirika la habari la ISNA limeripoti habari hiyo leo na kuongeza kuwa, taasisi hiyo maalumu ya kulinda usalama wa Libya chini ya amri ya baraza la uongozi la nchi hiyo imetoa tamko na kusema kuwa, imejitenga na baraza hilo pamoja na vikosi vingine vyote vya ulinzi vya serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya kama njia ya kulinda kile ilichodai ni hadhi yake ya kisheria.
Tamko la taasisi hiyo imedai kuwa, viongozi walioko madarakani nchini Libya wananuka ufisadi na baraza la uongozi wa nchi hiyo limeshindwa kuwadhibiti na hivyo kusababisha kuporomoka ubora wa huduma kwa jamii, kusambaratika taasisi za serikali na kushtadi migogoro ya kiuchumi na kiusalama.
Vile vile imesema kuwa, maafikiano ya kisiasa yaliyofikiwa nchini Libya ni maafikiano maovu na kuionya mirengo yote ya ndani na nje ya nchi hiyo, isijaribu kukwamisha kuundwa Libya ya kidemokrasia.
Taasisi hiyo muhimu ya kiusalama ya Libya imeongeza kuwa, wananchi wa nchi hiyo wamedanganywa na maafikiano ya kisiasa na walidhani kuwa maafikiano hayo yatakuwa ni kwa manufaa yao, lakini ukweli wa mambo ni kuwa hayo ni makubaliano waliyotwishwa wananchi wa Libya kwa kutumia fedha na propaganda za vyombo vya habari.
Taasisi hiyo sasa imejiunga na serikali ya Tripoli iliyokuwa inaongozwa na Khalifa al Ghawil ambayo iliondoka mjini Tripoli ili kuruhusu serikali ya umoja wa kitaifa ifanye kazi zake kwa ufanisi.