Sisitizo la Tanzania la kupambana na biashara haramu mashariki mwa Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18517-sisitizo_la_tanzania_la_kupambana_na_biashara_haramu_mashariki_mwa_afrika
Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amesisitiza kupambana na biashara haramu katika eneo la mashariki mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2016 09:59 UTC
  • Sisitizo la Tanzania la kupambana na biashara haramu mashariki mwa Afrika

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amesisitiza kupambana na biashara haramu katika eneo la mashariki mwa Afrika.

Rais John Pombe Magufuli ambaye ameelekea nchini Kenya kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili, amesisitiza kwenye mazungumzo yake na Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta kuwa biashara yoyote haramu katika nchi za eneo la mashariki mwa Afrika itafuatiliwa kisheria.

Akizungumza na mwenyeji wake katika mkutano na waandishi wa habari katika ikulu ya Nairobi, Rais Magufuli amekanusha madai kuwa, utawala wake umekuwa ukijiweka mbali na majirani kwa kutoa kipaumbele kwa masuala ya ndani. Akiwa katika ziara yake ya kwanza huko Kenya tangu aingie madarakani, Rais wa Tanzania amebainisha kuwa amekuwa akiwasiliana mara kwa mara kwa njia ya simu na Rais Uhuru Kenyatta na kwamba anaendelea kuitambua Kenya kama mshirika nambari moja wa Tanzania barani Afrika. Ameongeza kuwa, ziara yake nchini Kenya imelenga kuboresha uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Tanzania na Kenya ni miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC. Jumuiya hiyo ya kieneo inaundwa na nchi sita ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Sudan Kusini ilipewa rasmi uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki mwanzoni mwaka huu katika kikao cha dharura cha EAC.

Rais Kenyatta akimlaki mgeni wake Rais John Magufuli wa Tanzania jijini Nairobi

Rais John Magufuli alisisitiza katika kikao cha dharura cha wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika Dar es Salaam kuwa, nchi za mashariki mwa Afrika zimeazimia kufanikisha kupatikana maslahi makubwa kwa ajili ya watu wa eneo hilo; na kwa msingi huo zinatilia maanani suala la kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa kama Umoja wa Ulaya.  Rais wa Tanzania ambaye ndiye Mwenyekiti wa kiduru wa Jumuiya ya EAC amepata umashuhuri nchini kwake kutokana na vita anavyoviendesha dhidi ya ufisadi nchini humo. Magufuli ambaye ameshika hatamu za kuiongoza Tanzania baada ya kushinda uchaguzi mwezi Oktoba mwaka jana ameweka katika ajenda yake ya kazi suala la kupambana na ufisadi serikalini na kuboresha uchumi wa nchi hiyo. Rais huyo wa Tanzania ameashiria umaskini na ukosefu mkubwa wa ajira kuwa ni changamoto kuu kwa Tanzania na kutilia mkazo pia kuandaliwa fursa mpya za ajira kwa kizazi cha vijana wa nchi hiyo hadi kufikia mwaka 2020. Weledi wa mambo wanaamini kuwa Rais John Magufuli ameamua kutumia njia na mbinu tofauti na marais wa kabla yake wa Tanzania huku akitaka yafanyike marekebisho ya kiuchumi na kijamii nchini. Inaonekana kuwa, akiwa sasa Mwenyekiti wa kiduru wa EAC, Rais wa Tanzania anataka kuangaliwa upya mikataba na makubaliano ya kibiashara yaliyofikiwa kati ya Tanzania na nchi nyingine.

Wakuu wa nchi za EAC katika kikao chao mwanzoni mwa mwaka huu jijini Arusha Tanzania

Aidha amewaahidi wananchi  kuwa Tanzania itakuwa na nafasi katika kukuza ushirikiano wa kieneo mashariki mwa Afrika. Katika hali ambayo Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wa Soko la Pamoja la Kusini na Mashariki mwa Afrika (COMESA), tunaweza kuwa na matarajio na nafasi chanya ya Tanzania katika eneo. Katika mazingira hayo, biashara haramu kama magendo ya binadamu, biashara ya mihadarati na au ya bidhaa muhimu ni kikwazo kikubwa katika njia ya ustawi na maendeleo ya uchumi wa nchi za mashariki na kusini mwa Afrika. Ni kwa sababu hiyo ndio maana Rais Magufuli amesisitiza katika safaeri yake nchini Kenya juu ya kupambana na aina yoyote ya biashara haramu katika eneo la mashariki mwa Afrika. Miaka miwili nyuma, wakuu wa nchi wanachama wa EAC walikubaliana kuasisi umoja wa fedha kati ya nchi hizo ambao utaandaa uwanja wa kukuza na kuimarisha biashara na sarafu ya pamoja katika kipindi cha miaka kumi ijayo. Kuasisi umoja huo wa fedha kati ya nchi wanachama wa EAC kunatathminiwa kuwa hatua moja mbele ya kuleta mshikamano zaidi na ushirikiano wa kieneo kati ya nchi hizo. Aidha hatua ya Rais Magufuli ya kuunga mkono kujiunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na jumuiya hiyo ya kieneo inaweza kuwa ni hatua chanya katika kuimarisha misingi ya taasisi hiyo.