UN yatadharidha kutokea mauaji ya kimbari Sudan Kusini
Mtaalamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuwa yumkini Sudan Kusini ikatumbukia katika mauaji ya kimbari kutokana na kushadidi mapigano ya kikabila nchini humo.
Katika kikao na waandishi wa habari mjini Juba hapo jana, Adama Dieng, mshauri maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kuzuia mauaji ya kimbari amesema kuwa, wimbi la mauaji ya kikabila linaloshuhudiwa nchini Sudan Kusini kwa sasa linatia wasiwasi. Amesema uchunguzi wao umebaini kuwa, mauaji ya kikabila kwa kutumia mapanga, wanawake kubakwa na kuteketezwa kwa moto nyumba za watu wa kabila moja ni dhihirisho kuwa mchakato wa kushuhudiwa mauaji ya kimbari nchini humo unatokota.
Mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, kuna udharura wa kufanyika mazungumzo kati ya viongozi wa makabila mawili makuu yanayohasiamana nchini humo ili kuzuia kutokea mauaji ya kimbari kama yale ya Rwanda mwaka 1994, ambapo watu karibu milioni moja waliuawa.
Huku hayo yakiarifiwa, vyombo vya usalama nchini humo vimefunga Idhaa ya Eye, moja ya vituo vya radio vya taifa ambavyo vimekuwa vikieneza ujumbe wa amani na utangamano katika nchi hiyo changa zaidi duniani, pasina kutoa sababu zozote.
Hii ni katika hali ambayo, Jumatano iliyopita Kenya ilianza kuondoa askari wake nchini humo kulalamikia hatua ya Umoja wa Mataifa kumuachisha kazi kamanda wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki aliyekua akisimamia kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS, Luteni Jenerali Johnson Ondieki.