Uganda yateua timu mpya kuongoza Tume ya Uchaguzi
(last modified Fri, 18 Nov 2016 08:12:36 GMT )
Nov 18, 2016 08:12 UTC
  • Uganda yateua timu mpya kuongoza Tume ya Uchaguzi

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameteua timu mpya ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi nchini humo EC, huku muda wa kuhudumu kwa makamishna wa sasa ukimalizika jana Alkhamisi.

Kwenye barua yake kwa Spika wa Bunge, Rebecca Kadaga, Rais Museveni amemteua Jaji wa Mahakama ya Rufaa Simon Mugenyi Byabakama kurithi mikoba ya Badru Kiggundu, ambaye amekuwa mwenyekiti wa EC kwa muda wa miaka 14.

Wengine walioteuliwa na Rais Museveni kuongoza Tume ya Uchaguzi Uganda ni Hajjat Aisha Lubega, ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Mwenyekiti huku Peter Emorut, Steven Tashobya, Profesa George Piwang na Mustapha Ssebaggala Kigozi wakipendekezwa kuwa makamishna wa tume hiyo.

Uchaguzi mkuu Uganda ulifanyika Februari mwaka huu 2016

Iwapo makamishna hawa wapya wataidhinishwa na bunge la Uganda, basi watajiunga na Justin A. Mugabi, kamishna ambaye muda wake wa kuhudumu katika EC haujamalizika.

Vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki vimekuwa vikipinga matokeo ya chaguzi hususan wa rais sambamba na kulalamikia kile vinachokitaja kuwa ukosefu wa uadilifu na uendeshaji mbaya wa tume hiyo.

Tags