Ukurasa mpya wa uhusiano baina ya serikali ya Misri na Ikhwanul Muslimin
Mabadiliko yanayoonekana katika siasa na vyombo vya mahakama nchini Misri yananaonesha kwamba, kuna uwezekano wa kushuhudiwa ukurasa mpya katika uhusiano wa serikali ya Misri na kundi la Ikhwanul Muslimin.
Juzi, tarehe 24 Novemba, Muhammad al Baltaji, mmoja wa viongozi wa kundi la Ikhwanul Muslimin la Misri alisisisitiza mbele ya mahakama moja ya nchi hiyo kuwa, kundi hilo halina uhusiano wowote na makundi ya kigaidi kama vile al Qaida na Daesh, bali tatizo lake pekee ni watawala wa Misri. Uhusiano wa Misri na Ikhwanul Muslimin kwa namna fulani ni suala la ndani ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Hata hivyo madhara ya kuharibika uhusiano wa pande hizo mbili yanafika hadi nje ya Misri. Matukio ya eneo hili nayo yanaathiri katika uhusiano wa serikali ya Misri na Ikhwanul Muslimin. Ushahidi wa jambo hilo unaonekana wazi katika matukio ya miaka ya hivi karibuni yaliyosababishwa na uhusiano wa serikali ya Misri na Ikhwanul Muslimin.
Katika miaka ya 2012 hadi 2014 kundi la Ikhwanul Muslimin lilikuwa na mchango mkubwa kwenye matukio ya ndani ya Misri. Kundi hilo lilishinda katika chaguzi mbili za Rais na Bunge mwaka 2012. Muhammad Morsi, mgombea wa Ikhwanul Muslimin alishinda urais katika uchaguzi wa mwaka huo, licha ya nchi kama Saudi Arabia kumwaga fedha nyingi za kuwasaidia kifedha na kwa vyombo vya habari wagombea wengine wapinzani wa Morsi kama vile Ahmad Shafiq.
Kuingia madarakani kundi la Ikhwanul Muslimin nchini Misri kulikuwa ni kwa madhara ya wanajeshi wasiopenda dini wa nchi hiyo pamoja na baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia. Jambo hilo lilileta maelewano ya namna fulani baina ya Saudi Arabia na wanajeshi masekula wa Misri na mfano wa wazi kabisa uhusiano huo ni jinsi Saudi Arabia ilivyosaidia na kuunga mkono haraka sana mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 2013 yaliyomngóa madarakani Rais Muhammad Morsi wa Ikhwanul Muslimin huko Misri.
Saudi Arabia iliwasaidia sana wanajeshi wa Misri kufanya mauaji makubwa dhidi ya raia Waislamu wa nchi hiyo kwa ajili ya kudhibiti hali ya mambo. Mara baada ya kupinduliwa Muhammad Morsi, nchi tatu za Saudi Arabia, Imarati na Kuwait zilianzisha wimbi kubwa la propaganda za kulitangaza kundi la Ikhwanul Muslimin kuwa ni la kigaidi. Ijapokuwa kidhahiri wimbi hilo lilionekana ni kwa ajili ya kuiunga mkono serikali ya Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri, lakini kwa hakika lengo la nchi hizo za Kiarabu lilikuwa ni kuichochea serikali ya el Sisi iwakandamize na iwafanyie ukatili mkubwa wafuasi wa Ikhwanul Muslimin. Mahakama za Misri nazo zilitoa hukumu za ajabu ajabu zilizoonesha wazi kuathiriwa na chembechembe za Uwahabi wa Saudia. Hukumu zilizotolewa na mahakama hizo zilikuwa ni za vifo na vifungo vya maisha dhidi ya viongozi wa Ikhwanul Muslimin.
Hata hivyo, muda haukupita ile ukweli ulianza kudhihiri na katika miezi ya hivi karibuni mizozo na mivutano baina ya Misri na Saudi Arabia imeongezeka, na wakati huo huo serikali ya Misri inaonekana sasa hivi kulegeza misimamo yake kuhusiana na Ikhwanul Muslimin kiasi kwamba hata kuna uwezekano wa kuanza ukurasa mpya wa uhusiano wa pande hizo mbili.
Miongoni mwa ishara za jambo hilo zilionekana katikati ya mwezi huu wa Novemba. Wakati mwaka jana mahakama ya Misri ilimuhukumu kifo rais aliyepinduliwa Muhammad Morsi katika ile kesi iliyojulikana kwa jina la "kushambulia jela," mahakama ya rufaa ya Misri ilibadilisha hukumu hiyo mwezi huu wa Novemba na kufuta adhabu ya kifo dhidi ya Morsi na watuhumiwa wengine wote wa kesi hiyo.
Matamshi ya hivi sasa ya Muhammad al Baltaji ya kwamba Ikhwanul Muslimin haina uhusiano wowote na magenge ya kigaidi, bali ugomvi wake pekee ni watawala wa Misri, ni aina fulani ya ishara ya kuanza ukurasa mpya katika uhusiano wa serikali ya Misri na Ikhwanul Muslimin. Ni jambo lisilo na shaka kwamba, kama ukurasa huo mpya utafunguliwa, basi sababu ya kufunguliwa kwake haitakuwa kitu kingine ghairi ya kupungua kiwango cha uingiliaji wa Saudi Arabia katika masuala ya ndani ya Misri.