Amnesty 'yashtushwa' na mauaji ya halaiki nchini Uganda
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limelaani kile lilichokitaja kuwa mauaji ya halaiki katika eneo la Rwenzori, kusini magharibi mwa Uganda.
Abdullahi Halakhe, afisa wa Amnesty International katika kanda ya Afrika Mashariki amesema picha kamili ya mauaji hayo haijawekwa wazi na kuongeza kuwa, ukatili huo ni wa kutisha, usio na mfano na uliokiuka haki za binadamu.
Afisa huyo wa shirika hilo la kutetea haki za binadamu limeitaka serikali ya Rais Yoweri Museveni kuanzisha uchunguzi huru na usioegemea upande wowote juu ya mauji hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki katika mji wa Kasese ulioko katika mpaka wa nchi hiyo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Wapiganaji 46 wanaounga mkono mfumo wa kifalme nchini Uganda na maafisa polisi 16 waliuawa katika mapigano hayo.
Ripoti za kiusalama zinasema kuwa, kundi hilo lenye silaha linaendesha mapigano yenye lengo la kujitenga eneo la Rwenzururu na kuwa na mamlaka yake.
Vyombo vya usalama vya Uganda vimemtia mbaroni Charles Wesley Mumbere, mfalme wa Rwenzururu, ambaye vinamtuhumu kwamba, amekuwa akichochea machafuko hayo, madai ambayo mfalme huyo ameyakanusha.