Nov 30, 2016 15:26 UTC
  • Uganda yatakiwa kuchunguza mauaji ya Kasese na kumuachia huru mfalme

Vyombo vya usalama nchini Uganda vimeendelea kushutumiwa kwa mauaji ya watu wa mji wa Kasese katika eneo la Rwenzori, huku vyama vya upinzani vikiitaka serikali ya Kampala kumuachia huru mfalme wa eneo la Rwenzururu ambaye anatuhumiwa kuwaongoza waasi katika makabiliano dhidi ya maafisa usalama.

Patrick Tumwine, Mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu nchini Uganda la Human Rights Network (HURINET) ameitaka serikali kuunda Kamisheni ya Uchunguzi ya kutafuta kiini cha mauaji ya Kasese ya watu zaidi ya 100.

Amenukuliwa na gazeti la serikali la New Vision akisema kuwa, jopo huru la uchunguzi na lisiloegemea upande wowote linafaa kuundwa ili kuchunguza mauaji hayo ya hivi karibuni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo tangu mwaka 2014.

Maafisa usalama wa Uganda wakipiga doria mjini Kasese

Wakati huo huo viongozi wa kidini nchini Uganda wamesema kuna haja ya kufanyika mazungumzo ili kupatikana suluhu ya kudumu katika mzozo wa mfumo wa Kifamle nchini humo.

Huku hayo yakiripotiwa, Nobert Mao, mkuu wa chama cha upinzani cha DP ametoa mwito wa kuachiliwa huru mara moja na bila masharti, Mfalme wa Rwenzururu, Charles Wesley Mumbere, ambaye anazuiliwa na vyombo vya usalama kwa madai ya kuchochea machafuko ya Kasese.

Haya yanajiri masaa machache baada ya serikali ya Kampala kupitia Jeje Odongo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki kukanusha tuhuma zilizowasilishwa kwa serikali na Amnesty International kuwa imefanya mauaji ya kiholela nchini humo.

Mfalme wa Rwenzururu, Charles Wesley Mumbere,

Makumi ya wafuasi wa Mfalme Mumbere wanaounga mkono mfumo wa kifalme nchini Uganda pamoja na maafisa 16 wa polisi waliuawa katika mapigano hayo yaliyotokea mwishoni mwa wiki kwenye mji wa Kasese katika mpaka wa Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tags