UN yatahadharisha kuhusu mauji ya kimbari Sudan Kusini
Mjumbe wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini amesema baada ya kuitembelea nchi hiyo kuwa, kumetokea mauaji ya kimbari katika maeneo kadhaa ya Sudan Kusini.
Shirika la habari la IRIB limeripoti habari hiyo leo na kumnukuu Yasmin Sooka akisema hayo mjini Geneva Uswisi baada ya kurejea kutoka safari ya siku 10 ya kuitembelea Sudan Kusini kwamba mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini humo yanafanana na yale yaliyotokea mwaka 1994 nchini Rwanda. Amesema, mauaji ya kimbari Sudan Kusini yametokea kwa mfululizo na kuna uwezekano hali ya nchi hiyo ikawa sana na ile ya Rwanda mwaka 1994.
Mjumbe huyo wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini ametanabahisha kuwa, vitendo kama vya kuwanyima watu chakula, kuwanajisi watu kwa umati na kuchoma vijiji ni katika mambo yanayoonesha kuwa, kuna mauaji ya kimbari yanaendelea hivi sasa Sudan Kusini.
Sooka amesisitiza kuwa, mazingira yaliyopo yanaonesha kwamba, Sudan Kusini inaelekea kuwa Rwanda nyingine na kwamba jamii ya kimataifa ina jukumu la kuchukua hatua za haraka za kuzuia jambo hilo.
Tangu mwezi Disemba 2013 wakati ulipoanza mgogoro baina ya Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar, raia milioni tatu wa Sudan Kusini wamekuwa wakimbizi. Wakimbizi milioni moja na laki tisa wanakadiriwa kukimbilia maeneo mengine ndani ya nchi hiyo na wengine wamekimbilia nchi jirani.