Jeshi la serikali Libya ladhibiti kikamilifu mji wa Sirte
Vikosi vya jeshi la Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya vinaudhibiti kikamilifu mji wa Sirte kaskazini mwa Libya.
Msemaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya amesema kuwa vikosi vya jeshi la serikali hiyo vinaudhibiti kikamilifu mji wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo. Ridha Issa amesema kuwa vikosi vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa sasa vinaudhibiti kikamilifu mji wa Sirte baada ya kupambana na kundi la kigaidi la Daesh kwa muda wa miezi sita. Ameongeza kuwa wapiganaji wa kundi la Daesh wamefurushwa kikamilifu.
Mji wa Sirte uliopo katika pwani ya Bahari ya Mediterania ni eneo muhimu la mwisho lililokuwa likishikiliwa na kundi la kigaidi la Daesh nchini Libya.
Vikosi vya jeshi la serikali ya Libya tarehe 12 mwezi Mei mwaka huu vilianzisha oparesheni ya kijeshi ya kuukomboa mji wa Sirte na kufanikiwa kuyakomboa maeneo mengi ya mji huo kwa haraka. Hata hivyo kundi la Daesh lilikuwa likijilinda na kujibu mashambulizi hayo kwa kutumia magari yanayotegwa mabomu, walenga shabaha na kutumia pia mabomu ya kutengeneza kwa mkono.